
………………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu, Kiteto
WADHAMINI wawili waliomdhamini mshtakiwa Moita Tepeno aliyejipatia fedha kwa kutumia jina la Mkuu wa Wilaya ya Kiteto Mkoani Manyara, Kanali Patrick Songea, wamepelekwa mahabusu baada ya mshtakiwa huyo kutoroka.
Wadhamini hao wawili Munjuri Tepeno na Leshoni Moita walimdhamini Tepeno kwenye kesi hiyo namba 122/2020 kwa sh500,000 kila mmoja, walishindwa kulipa fedha hizo na kupelekwa mahabusu gereza la Kiteto.
Hakimu mkazi mfawidhi wa mahakama ya Wilaya ya Kiteto, Mossy Sasi akizungumza jana mahakamani hapo aliamuru wadhamini hao wawili wa kesi hiyo ya jinai waende mahabusu hadi Machi 15 mwaka huu.
Hakimu aliwataka wadhamini hao wawili watoe fungu la dhamana ya sh500,000 kwa kila mmoja baada ya mshtakiwa kuruka dhamana wakashindwa kulipa na kupelekwa mahabusu.
Awali, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu amesema walimfikisha mahakamani hapo Tepeno ambaye ameruka dhamana na kumfungulia shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Makungu amesema Tepeno alijipatia sh500,000 kwa njia ya udanganyifu kwa kutumia vibaya jina la mkuu wa wilaya hiyo Keepanali Songea kinyume na kifungu cha 302.
Amesema pia kosa hilo lililofanywa na mshtakiwa huyo ni kinyume cha kifungu cha 301 vyote viwili vya kanuni ya adhabu ya sura ya 16.
Amesema Tepeno alijipatia sh500,000 baada ya kumrubuni raia mwema kuwa anampelekea Kanali Songea baada ya binti yake mwanafunzi kupata ujauzito alipokuwa kwenye likizo ya corona mwaka jana.
“Binti huyo alikuwa anasoma mkoani Arusha na akapata ujauzito huo wilayani Kiteto wakati shule na vyuo vikiwa vimefungwa mwaka jana kwenye janga la corona,” amesema Makungu.
Amesema TAKUKURU wanaendelea kumtafuta Tepeno na wanaomba wadau wa mapambano dhidi ya rushwa popote watakapomuona wawafahamishe ili aweze kukamatwa kwenda kupambana na kesi yake.
“Rai yetu kwa watanzania kuacha tabia za kuwadhamini washtakiwa wasio waaminifu kwa kuwa sheria inasema ukishindwa kutekeleza wajibu wa kuhakikisha unamleta mahakamani mshtakiwa uliyemdhamini utalipa faini,” amesema Makungu.
Amesema inabidi ukipe fungu la dhamana uliloahidi au uiache familia yako na kulazimika kwenda kutumikia kifungo.