Home Michezo NAMUNGO FC YAANZA VIBAYA CAF YACHAPWA 1-0 NA RAJA CASABLANCA

NAMUNGO FC YAANZA VIBAYA CAF YACHAPWA 1-0 NA RAJA CASABLANCA

0
TIMU ya Namungo FC imeanza vibaya mechi zake za Kundi D Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuchapwa 1-0 na wenyeji, Raja Club Athletic leo Uwanja wa Mohamed V Jijini Casablanca nchini Morocco. 
Bao lililoizamisha Namungo FC inayofundishwa na kocha Hemed Morocco leo limefungwa na Soufiane Rahimi dakika ya 54 kwa penalti kufuatia beki Carlos Protas kuunawa mpira kwenye boksi. 
Refa Hassen Corneh wa Liberia aliyekuwa anasaidiwa na Boris Ditsoga na Felix Abaa Eyaga wote wa Gabon alimtoa kwa kadi nyekundu beki wa Namungo FC, Ramadhani Haruna Shamte kufuatia kumuonyesha kadi mbili za njano dakika ya 22 na 66.
Kwa matokeo hayo, Nakmungo FC inaanzia nafasi ya tatu kwenye kundi hilo kufuatia wenyeji wengine, Pyramids kuwachapa Nkana FC ya Zambia 3-0, mabao ya Mahmoud Wadi dakika ya pili, Islam Issa dakika ya tisa na Mohamed Farouk dakika ya 90 na ushei Uanja wa Jeshi la Anga wa Juni 30 Jijini Cairo, Misri. 
Sasa Pyramids wanaanzia kileleni, wakiizidi wastani wa mabao Raja, wakati Namungo ni ya tatu na Nkana FC ikashika mkia. 
Mechi zijazo, Namungo FC watakuwa wenyeji wa Pyramids Machi 17 Uwanja wa Azam Complex, Chamazi Jijini Dar es Salaam na Nkana FC watawaalika Raja Casablanca Uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola, Zambia.