Na Dotto Mwaibale, Singida.
HALMASHAURI ya Wilaya ya Ikungi mkoani Singida katika kipindi cha miaka miwili na nusu imefanikiwa kutoa mikopo zaidi ya sh. milioni 200 huku wanawake wakiwa ni wanufaika wakubwa.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Justice Kijazi wakati akizungumza katika kilele cha maadhimisho ya siku ya wanawake duniani yaliyofanyika juzi.
Alisema katika fedha hizo nyingi zilikopwa na wanawake hivyo alitoa rai kuwa wanawake ni warejeshaji wazuri wa mikopo kuliko makundi mengine lakini hata katika makundi hayo ndani yake kuna wakina mama.
” Nipende kusema kuwa mikopo mingi katika halmashauri inaenda kwenye kundi ili la wakina mama.” alisema Kijazi.
Kijazi alisema lengo la mikopo hiyo ni kutaka izalishwe hivyo aliwaomba wakina mama hao pindi wakikopeshwa waizalishe.
Aidha Kijazi alisema kwa kutambua kuwa mama yeye ni mtunzaji wa familia na ukimuelimisha utakuwa umeelimisha familia nzima.
” Natambua kazi kubwa wanayoifanya wakina mama kwenye kuendeleza taifa letu kwani wao ni nguzo ya jamii inayotuzunguka ni jambo moja tu tunalotakiwa kulifanya sio kuwawezesha bali ni kuwaonesha fursa za maendeleo kwa sababu wanaweza.” alisema Kijazi.
Kijazi alitoa ahadi kuwa iwapo Rais Dkt.John Magufuli ataona aendelee kukaa Ikungi atakuwa nao bega kwa bega.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Edward Mpogolo akinukuu baadhi ya maneno yaliyopo kwenye biblia alisema mwanamke ni mzazi, mlezi, mlinzi, muombezi na msaidizi kama ilivyo andikwa katika kitabu cha Mwanzo 2:18 hivyo anapaswa kuthaminiwa.
Aidha Mpogolo alisema wanawake wana nguvu na uwezo mkubwa ndio maana wanaweza kugombea nafasi mbalimbali lakini akatoa angalizo kuwa katika siasa wanavutana wenyewe mmoja akipanda ngazi na kufika juu mwingine anamvuta ashuke chini badala ya kupeana mkono.
Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Ikungi, Haika Massawe alisema jitihada za halmashauri hiyo za kumwezesha mwanamke zinaungwa mkono na wadau wa maendeleo ambapo mashirika ya kimataifa na Asasi za kiraia zimeendelea kuwawezesha wanawake.
Alisema UN Women na watekelezaji wa miradi hiyo (Farm Africa, TAHA, Kiwohede na C-Sema) wanatekeleza mradi wa kuimarisha usawa wa kijamii kwa kuwajengea uwezo wanawake katika kilimo, umiliki wa rasilimali na kupinga ukatili wa kijinsia.
Massawe aliyataja mashirika mengine yanayounga juhudi hizo za Serikali kwa kundi hilo kuwa ni SEMA- Singida, SPRF-Singida, NODIP, OVCCT na SMCCT.