Meneja wa Benki ya Nmb kanda ya kusini Janeth Shango wa tatu kushoto na meneja wa benki hiyo tawi la Namtumbo Atu Mwanjejele wa pili kushoto na Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Sofia Kizigo wa nne kutoka kushoto wakimwagalia kwa furaha mkazi wa Namtumbo Siwetu Pili aliyelala katika moja ya vitanda vya kulaza wagonjwa vilivyotolewa na nmb kwa Hospitali ya wilaya Namtumbo jana,ambapo jumla ya vifaa vyenye thamani ya milioni 10 vimetolewa na Benki hiyo,kushoto ni Mganga Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Dkt Lucia Kafumo,
****************************************
BENKI ya NMB, imekabidhi msaada wa vifaa mbalimbali kwa Hospitali ya wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma vyenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 10 ili viweze kusaidia kuboresha utoaji huduma kwa wananchi.
Vifaa vilivyotolewa ni vitanda 5 vya wagonjwa,vitanda viwili vya kujifungulia,shuka 25 ambapo vinakwenda kupunguza uhaba wa vitanda katika Hospitali hiyo ambayo imeanza kulaza wagonjwa vilikabidhiwa kwa Mkuu wa wilaya hiyo Sofia Kizigo.
Akizungumza wakati wakati wa makabidhiano ya vifaa hivyo meneja wa benki ya Nmb kanda ya Kusini Janeth Shango alisema,Benki hiyo ipo mstari wa mbele katika kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano ya kuboresha na kuimarisha sekta ya Afya hapa nchini.
Kwa mujibu wa Shango ingawa Serikali inafanya makubwa, hata hivyo Nmb kama wadau ina wajibu wa kuunga mkono juhudi hizo za maendeleo kwa kusaidia jamii na msaada huo ni sehemu ya faida inayoipata kila mwaka ambapo kwa zaidi ya miaka nane mfululizo imechangia asilimia 1 ya faida kama sehemu ya uwajibikaji kwa jamii.
Alisema, wanaamini vifaa hivyo vitawezesha wananchi wa wilaya hiyo na wale wanaotoka maeneo mengine ya nchi kupata huduma bora pindi wanapofika kupata matibabu.
Shango alisema, benki hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za wadau wake wakubwa katika kuhakikisha kuwa changamoto za kijamii zinapatiwa ufumbuzi katika kujenga afya bora na elimu bora kwa jamii ya Kitanzania.
Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Sofia Kizigo, ameishukuru benki ya Nmb kwa msaada huo kwani vinakwenda kuimarisha utoaji huduma bora za afya kwa watumishi wa sekta ya afya na kupata huduma bora za matibabu kwa wananchi.
Alisema, hii ni mara ya pili kwa Nmb kutoa msaada kwani mara ya kwanza ilichangia fedha kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya wilaya kupitia Namtumbo Marathoni.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa wilaya ya Namtumbo Dkt Lucia Kafumo ameishukuru serikali ya awamu ya tano kwa kutoa shlingi bilioni 1.8 kwa ajili ya ujenzi wa majengo wa Hospitali ya wilaya ambao umekamilika kwa asilimia 98.
Alisema, mwaka jana walianza kutoa huduma mbalimbali ikiwemo kulaza wagonjwa ambapo walikuwa na vitanda 25 tu,kwa hiyo kupatikana kwa vitanda hivyo vinakwenda kupunguza uhaba wa vitanda katika Hospitali hiyo.