Mkurugenzi Mtendaji wa Klabu ya Simba Barbara Gonzalez akizungumza na wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa sherehe ya kuadhimisha siku ya wanawake Duniani iliyofanyika tarehe 08/03/2021 katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa chama cha wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angella Muhozya akiwapongeza wanawake wa JKCI kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kutoa huduma kwa wagonjwa wanaotibiwa katika taasisi hiyo wakati wa sherehe ya kuadhimisha siku ya wanawake Duniani iliyofanyika tarehe 08/03/2021 katika Taasisi hiyo.
Mtaalam wa afya ya Jamii kutoka Doctor’s Plaza Polyclinic Sophia Byanaku akiwapa motisha wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa sherehe ya kuadhimisha siku ya wanawake Duniani iliyofanyika tarehe 08/03/2021 katika Taasisi hiyo.
Mchungaji kutoka kanisa la New Day Church Rose Shaboka akizungumza na wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati wa sherehe ya kuadhimisha siku ya wanawake Duniani iliyofanyika tarehe 08/03/2021 katika Taasisi hiyo.
Baadhi ya wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakifuatilia mada mbalimbali zilizokuwa zikiendelea wakati wa sherehe ya kuadhimisha siku ya wanawake Duniani iliyofanyika tarehe 08/03/2021 katika Taasisi hiyo.
Wataalam wa afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKIC) ambao walishiriki katika maonesho ya mavazi wakati wa sherehe ya kuadhimisha siku ya wanawake Duniani iliyofanyika tarehe 08/03/2021 katika Taasisi hiyo.
Baadhi ya wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakiwa katika picha ya pamoja na wageni waalikwa wakati wa sherehe ya kuadhimisha siku ya wanawake Duniani iliyofanyika tarehe 08/03/2021 katika Taasisi hiyo.
Picha na: JKCI
*************************************
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
10/3/2021 Wahudumu wa afya nchini wametakiwa kufanya kazi yao ya kuokoa maisha ya wagonjwa kwa kumtanguliza Mungu kwanza kwani wamebeba dhamana ya maisha ya watu.
Wito huo umetolewa hivi karibuni na mchungaji Rose Shaboka wa kanisa la New Day Church wakati akizungumza na wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika sherehe ya maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani yaliyofanyika katika Taasisi hiyo.
Mchungaji Rose alisema wahudumu wa afya ni watu wa muhimu sana katika jamii na hata biblia inawatambua kutokana na huduma ya matibabu wanayoitoa hata Luka ambaye alikuwa mwanafunzi wa Yesu alikuwa ni tabibu.
“Dhamana ya uhai wa maisha ya watu mliyoibeba ni kubwa,kama mtakosea kumtibu mgonjwa na kumpa dozi isiyo sahihi atapoteza maisha fanyeni kazi yenu mkijua kuwa mnamtumikia Mungu ambaye atawalipa kutokana na huduma mnayoitoa”,.
“Kataeni kutumika kufanya mambo ambayo ni kinyume na maadili yenu ya kazi kama vile Farao alivyotaka kuwatumia wakunga kuwaua watoto wa kiume wa Israel wakati wanawazalisha wanawake wa kiebrabia lakini wakunga hao walikataa na kufuata taratibu zao za kazi na hawakuwaua watoto wale”, alisema Mchungaji Rose.
Alisema amekuwa akifurahia kuwasaidia watoto wanaotoka katika familia zisizokuwa na uwezo na kuwalipia gharama za matibabu kwani yeye ni mama na ana watoto ndiyo maana anasaidia watoto tangu mwaka 2020 alianza kutoa huduma hiyo.
Mchungaji Rose pia aliwaambia kina mama hao kuijuilsha jamii inayowazunguka siyo magonjwa yote yanaponywa katika maombi bali kuna magonjwa mengine ni lazima yatibiwe katika vituo vya kwani hivi sasa kuna maadhi ya watu wanafikiri wakiumwa watapona Kanisani na siyo Hospitali.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa klabu ya Simba Barbara Gonzalez alisema mwanamke akipewa nafasi ya uongozi anaweza kuongoza na kupata mafanikio mazuri hii ni kutokana na changamoto mbalimbali za maisha wanazokabiliana nazo kila siku.
Barbara alisema wakati anaanza kufanya kazi katika klabu hiyo kubwa barani Afrika kuna baadhi ya watu walimbeza na kusema hataweza kufanya kitu chochote lakini kwa miezi michache aliyofanya hapo mafanikio makubwa yamepatikana ameonesha anawezana ataendelea kusonga mbele.
“Jambo la muhimu ni kutokukata tamaa angalia watu wengine wanaofanya vitu vizuri jifunze kutoka kwao, siyo kitu rahisi kufanya kazi wewe ndiye unayetengeneza mazingira na mahusiano mazuri na wenzako vitu ambavyo vitakufanya ufanikiwe”, .
“Nitakuwa mfano kwa wasichana wadogo nitajitahidi kuwasaidia ili wajifunze kutoka kwangu na kupata uzoefu hii itawafanya waweze kujiamini na kuamini hapo baadaye watakuwa viongozi wazuri”,alisema Barbara.
Alisema katika sekta ya michezo nchini na Barani Afrika klabu ya Simba ni mfano mzuri wa kuigwa kwa kuwajali wanawake na kuwapa uongozi yeye akiwa ni mfano mmojawapo na hivi karibuni walimchagua mwanamke kuwa kiongozi wa Simba Queens ambaye wanaamini atakuza sekta hiyo ya mpira wa miguu kwa wanawake.
Naye mtaalamu wa Afya ya Jamii kutoka Doctor’s Plaza Polyclinic Sophia Byanaku aliwapongeza wanawake wa hao wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete kwa kazi ngumu wanayoifanya ya kuokoa maisha ya watu.
Sophia alisema jambo la muhimu ni kuwaelimisha wanawake wanaotibiwa au kuuguza ndugu zao wanaotibiwa katika Taasisi hiyo kutumia mitandao ya kijamii kufanya mambo yenye tija ambayo yatawaletea mafanikio katika familia zao.
“Hivi sasa wanawake wengi wanacheza michezo mbalimbali ya fedha hii ikiwa ni pamoja na ujenzi , kununua vyombo, nguo na vitu vingine lakini wakipata matatizo ya kiafya wanakosa kupata huduma kwa wakati kwa kuwa hawana bima za afya”,.
“Wakati umefika sasa tuwaelimishe wanawake wenzetu wacheze pia michezo ya kuchangiana fedha kwa ajili ya kukata bima za afya ili pindi watakapoumwa waweze kupata huduma za matibabu kwa wakati kuliko kuanza kuchangisha fedha za kusaidiwa kulipia gharama za matibabu”, alisisitiza Sophia.