Maelekezo hayo yalitolewa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Magu, Zablon Makoye kwa niaba ya wajumbe wa kamati hiyo saiasa baada ya kuhitimisha ziara hiyo.
Alisema miradi ya maji na umeme katika kijiji cha Kabale iliyokuwa ikitekelezwa na wazabuni kabla ya mikataba yao kuvunjwa na serikali na kukabidhiwa wataalamu wa ndani,waikamilishe haraka na kwa weledi ili iwanufaishe wananchi.
“Natoa maelekezo, vijiji 10 wilayani Magu bado havijaunganishiwa umeme na hapa Kabale, wahamasisheni wananchi walio jirani na miundombinu ya umeme inakopita waunganishwe,”alisema Makoye.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Kabale, Ruben Yakob, alisema zaidi ya wananchi 28 walilipia fedha lakini hadi sasa hawajaunganishiwa umeme.
Kaimu Meneja wa Tanesco Wilaya ya Magu, Hamis Mkima, alisema baadhi ya wananchi hawakufikiwa na huduma hiyo baada ya kampuni ya NIPO kuvunjiwa mkataba,hivyo serikali ina tathmini kazi na uhakiki wa malighafi alizotumia mkandarasi huyo ili kampuni ya ATDECO iendelee na kazi.
“Mkandarasi alifanya km 2.0 sawa na asilimia 14 ya mradi huu akavunjiwa mkataba,kazi hiyo sasa itafanywa na kampuni ya tanzu ya Tanesco lakini ipo changamoto hapa Kabale ni wateja 8 tu waliounganishwa kwenye njia moja ya msongo mdogo wa umeme (Single phase),”alisema.
Kuhusu maji, Meneja wa RUWASA Magu, Mhandisi Anna Mbawala, alisema mradi wa maji Kabale uliogharimu sh.milioni 231 utawanufaisha watu 5,000 na utaanza kusambaza maji safi na salama,ifikapo Machi 16, mwaka huu.
“Mradi huu haukukamilika mapema sababu ya kuchelewa kwa manunuzi ya pump na kangavuke (jenereta),kwa sasa tuko kwenye majaribio,kitanda cha tenki la maji ujazo wa lita 75,000 na vituo 8 kati ya 10 vya kuchotea maji vimekamilika,”alisema.
Baadhi ya wananchi wa kijiji hicho, Simon Kafaransa na Yunge Makoye, waliishukuru serikali kwa kuwaletea mradi wa maji safi na salama ya bomba,wataondokana na adha ya kunywa na kutumia maji ya kwenye malambo.
“Tulikuwa tukichangia maji pamoja na mifugo,lakini sasa mradi huu umetuondoa kwenye shida ya maji hasa wakati wa kiangazi na tunaishukuru sana serikali,”alisema Yunge.
Aidha Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kalli, alisema baada ya maelekezo ya kamati ya siasa watumishi wa serikali wafanye kazi kwa maslahi ya wananchi,waishi na shida za watu na kuwaletea maendeleo.