*************************************
~ Wahamasika kusimamia miradi ya ujenzi ya kimaendeleo.
~ Shilatu aunga mkono ujenzi.
Na Mwandishi wetu Mihambwe
Wananchi wa kata ya Michenjele iliyopo Tarafa ya Mihambwe wamepewa darasa fupi ya namna ya kusimamia ujenzi wa miradi ya kimaendeleo.
Wananchi hao ambao wanajitolea nguvu kazi zao kwenye ujenzi wa Madarasa mawili na ofisi moja kwenye shule ya msingi ya Michenjele wameaswa kuzingatia BOQ na vipimo husika vya ujenzi vilivyopo kwa mujibu wa BOQ.
“Nimejifunza mengi kutokana na darasa hili fupi tulilopatiwa hapa kwenye mradi, litatuimarisha kwenye usimamiaji wa miradi ya ujenzi ambayo inajengwa kwa nguvu ya kodi zetu.” Alisema Ally Mohamed Ucheche ambaye ni Mwananchi wa kijiji cha Shangani kilichopo kata ya Michenjele
Hayo yamejitokeza leo Jumanne Machi 9, 2021 kwenye ziara aliyoifanya Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu ya kukagua maendeleo ya mradi huo wa ujenzi na kutoa fursa kwa fundi mkuu kuwafundisha Wananchi namna ya kuzingatia vipimo na usomaji wa BOQ.
“Nawapongeze Wananchi kwa namna walivyohamasika kuunga mkono ujenzi kwa mfumo wa force account ambapo Wananchi wanajitolea nguvu kazi zao na ndio wasimamizi wa mradi kwa ushirikiano na kamati za ujenzi wa mradi husika. Lakini pia nimewaelekeza wazingatie BOQ na wamepata darasa fupi la namna ya kuisoma BOQ, kusoma vipimo vya ujenzi na namna kamati za ujenzi zinavyofanya kazi kwa ushirikiano. Lengo kuu ni kuhakikisha miradi inakamilika kwa ubora unaolingana na thamani ya fedha husika.” Alisisitiza Gavana Shilatu mara baada ya kumaliza ziara yake.
Gavana Shilatu pia alikagua na kushiriki ujenzi mradi huo ambao upo kwenye hatua ya umwagaji zege la msingi na kusisitiza ujenzi wenye ubora unaolingana na thamani ya fedha na mradi kukamilika kwa wakati.
Katika ziara hiyo Gavana Shilatu aliambatana na Mtendaji kata Michenjele, Afisa Elimu Kata na kupokelewa na Mwalimu mkuu shule ya msingi Michenjele, wenyeviti wa vijiji, kamati za ujenzi na Wananchi ambao wanajitolea kutoa nguvu kazi zao na kusimamia mradi huo.