********************************************
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Jumuiya ya wanawake wa shule ya msingi Green Acres wamesherekea siku ya wanawake dunia kwa kupanda miti ikiwa ni sehemu ya kuwakumbusha wanawake kuwa pamoja na jitihada nyingi za kimaendeleo wasisahau kutunza mazingira yao.
Akiongea na waandishi wa habari katika maadhimisho hayo mkurugenzi wa shule hiyo Frazierh Ngalesoni alisema kuwa mazingira yanaleta madhari nzuri na hewa ambapo ili kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabia ya nchi wao wameona ni vyema wakasherehekea siku ya wanawake kwa kutunza mazingira ambapo pia wanaamini ni jukumu la wanawake.
“Mazingira ndio kila kitu hivyo nawaasa kila mtu ajikite kuyatunza kwa kupanda miti angalau miti ya kivuli, matunda na hata maua mara moja moja na mwaka utakapofikia ukiongoni mtaona ni kwajinsi gani mmeisaidia dunia kuondokana na athari za tabaka la Ozone,Alisema Mrs Ngalesoni.
Aidha aliwataka wanawake kutokata tamaa hata kama waume zao hawapo kwani daima wao ndio nguvu ya familia na wana shughuli nyingi za kufanya ili familia zao ziweze kusimama na kuwa bora.
“Nijitolee mfano mimi mwenyewe haikuwa njia rahisi kufika hapa nilipo, nianzisha shule hii mwaka 1991 sebuleni kwangu nikiwa na wanafunzi watano tuu lakini hivi sasa shule yangu ni kubwa inawanafunzi zaidi ya 1400 na kitaaluma pia tuko vizuri kwahiyo niwatie moyo wanawake wenzangu hakuna kitu kinakuja kirahisi lakini pia hupaswi kukata tamaa bali unatakiwa kukaza hadi utakapofanikiwa,” Alisema.
Mwalimu Kirita wa shule hiyo Alisema kuwa wameadhimisha kwa kupanda miti kwasababu wanaamini ukitunza mazingira na yenyewe yanakutunza ambapo pia wamewashirikisha wanafunzi wa kike kwasababu wanajua kuwa ukimwelimisha mwanamke umeielimisha jamii nzima.
“Pamoja na kwamba tunawalea wanafunzi wetu kimaadili na kimasomo lakini pia tumependa tuwaonyeshe kuwa kuna upande mwingime unaomtegemea mwanamke nayo ni mazingira ili wayatunze kwanzia sasa wakiwa hapa shuleni, majumbani kwao na hata baadae watakapofikia kuanzisha familia wajue kuwa jukumu la kutunza mazingira ni la mama,” Alisema mwl Kirita.
Kuhusiana na wanawake wengine Alisema kuwa katika kipindi cha sasa hakutakiwi kuwepo kwa mwanamke anayelala hasa katika masuala ya kiuchumi pamoja na kwamba wanamajukumu makubwa katika jamii ikiwemo malezi, wasikae badala yake watafute fursa za kimaendeleo kwani hakuna ambacho hawakiwezi.
Kwa upande wake mwalimu Miriam Hezron Mashauri alisema kuwa anaungana na wanawake wenzake kuunga mkono kauli mbiu ya mwaka huu isemayo “wanawake katika uongozi chachu kuleta dunia yenye usawa” hivyo wanawake wajitokeze kugombea nyanja mbalimbali za uongozi kwani wanapopata fursa ya kuwa viongozi wanapata nafasi ya kukemea maovu katika jamii.
Mwalimu Mashauria Alisema kuwa uongozi unaanzia kwenye familia zao kwa kuwakuza watoto wao wakike na wakiume kwa kuwafundisha kuwa wote ni sawa na hakuna kubagua jinsia na kwa kufanya hivyo hilo litaenea katika jamii nzima na watoto wakike watapata nafasi ya kutambua wajibu wao na kuwa wanaweza.
“Tunapopata nafasi za uongozi na kukemea maovu dhidi ya wanawake, watoto wa kike watakuwa na uwezo wa kufanya mambo mbalimbali katika ikiwa ni pamoja na kutambua kuwa wana majukumu sawa na watoto wa kiume hali itayowapa ujasiri na kuendelea kutimiza wajibu wao,”Alieleza mwl Mashauri.
Hata hivyo baadhi ya wanafunzi walisema kuwa walimu wanawake ndio wanaowalea ili waweze kuja kuwa wanawake bora hapo baadae ambapo kwa maadhimisho ya mwaka huu wamewafundisha kuwa pamoja na mwanamke kulea familia na kufanya shughuli za kujiingizia kipato lakini pia wanatakiwa kutunza mazingira.
Dianarose Mawala mwanafunzi wa darasa la tano alisema kuwa jambo hilo la upandaji miti walilolifanya katika kuadhimisha siku ya wanawake kunamfundisha yeye kuja kuwa mama bora wa familia na taifa lake kwani watafuata na kuyaheshimu yote waliyofundishwa na wanayoendelea kuwafundisha.
Esther Elisha Mella wa darasa la sita alisema kuwa shule yao ya Green Acres kila mwaka wanaadhimisha siku ya wanawake dunia kwa kufanya shughuli mbalimbali ambapo kwa mwaka huu wamepanda miti jambo ambalo linatufundisha kama wanawake wa baadae tutunze mazingira.
“Wanatufundisha kuja kuwa wanawake bora tutakaoweza kutunza familia zetu lakini pia kutunza mazingira yetu kwani mazingira ni kila kitu kinachotuzungua hapa duniani ambapo tumepanda miti ilituweze kupata hewa nzuri na afya zetu ziwe nzuri,” Alisema mwanafunzi Esther.