****************************************
Na Lusungu Helela-Morogoro
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro ameiagiza Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kuhakikisha inawarejesha Faru ambao walitoweka miaka ya 80 kutokana na kukithiri kwa vitendo vya ujangili katika Hifadhi hiyo.
Akizungumza leo mkoani Morogoro na Menejimenti ya Hifadhi hiyo, Dkt.Ndumbaro amesema kwa kuwa Faru hao walikuwepo kipindi cha nyuma lakini tatizo la ujangili lilipelekea faru hao kutoweka kabisa.
Amesema Hifadhi hiyo kwa sasa ina Wanyamapori wakubwa wa nne na sio watano ambao ni Simba, Tembo, Nyati na Chui. “Kwanini Faru hawapo katika Hifadhi hii, Je mazingira sio rafiki kwao” alihoji Dkt.Ndumbaro
” Katika uongozi wangu lazima nihakikishe Hifadhi ya Taifa ya Mikumi inakuwa “Big Five na sio Big Four ” , Menejimenti nataka kuwaona faru katika Hifadhi hii kwani naamini wanaweza kuishi” alisisitiza Dkt.Ndumbaro.
Amesema ikolojia ya Hifadhi yaTaifa ya Mikumi inaruhusu Faru kuweza kuishi katika eneo hilo ikizingatiwa kuwa kipindi cha nyuma waliishi, Hivyo kurejeshwa kwao kutasaidia Hifadhi ya Mikumi kuwa Hifadhi bora zaidi kwa vile itakuwa imesheheni kiu ya Watalii wenye matamanio ya kuona Wanyamapori wakubwa wote katika Hifadhi hiyo
Ameagiza kuwa mara baada ya faru hao kurejeshwa katika Hifadhi hiyo ni lazima ulinzi uimarishwe maradufu ili kosa lililotokea kipindi cha nyuma liisijirudie.
” Hakikisheni mnawafunga vifaa maalum vitavyowasaidia kuangalia mienendo yao ili kuwahakikishia usalama wao” alisisitiza Ndumbaro
Amesema kurejeshwa kwa faru hao ni ishara tosha kuwa tatizo la ujangili nchi nzima umepungua kwa asilimia 90 hivyo kuna usalama wa Wanyamapori wote wakiwemo faru watakaoletwa.
Kwa upande wake, Mtafiti wa kutoka Taasisi ya Utafi wa Wanyamapori Tanzania( TAWIRI) Dkt. Gabriel Ottawa amesema inawezekana faru watakaorejeshwa wataweza kuishi vizuri kwa vile kipindi cha nyuma faru hao walikuwepo katika Hifadhi hiyo
Ameahidi mbele ya Waziri kuwa watafanya kila liwezekanalo kwa kufanya tafiti mbalimbali kabla ya kuwaleta faru hao ili kujua changamoto pamoja na kuzitafuta ufumbuzi wa namna faru hao wakishaletwa waweze kuishi kwa usalama ili waweze kuendeleza kizazi katika Hifadhi hiyo.
Naye Kamishna Mwandamizi wa Kand ya Mashariki, Asteria Ndaga alikiri kuwepo kwa faru katika kipindi cha nyuma na hivyo kuahidi kuwa maelekezo aliyoyatoa Mhe.Waziri yatatelelezwa haraka na kwa umakini wa hali ya juu.