Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) Dkt. Elirehema Doriye akizungumza na wanawake wafanyakazi wa Shirika hilo (hawapo pichani) wakati wa maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani.
Meneja Rasilimali watu kutoka Shirika la Bima la Taifa (NIC) Bi. Venaranda Mpaze kulia akimkabidhi mahitaji mbalimbali mlezi wa kituo cha Yatima Group Trust Fund kilichopo Mbagala Chamanzi jijini Dar es salaam.
Mwanasaikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Dkt. Chris Mauki akizungumza na wanawake wafanyakazi wa NIC (wengine hawamo pichani) wakati wa maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani.
Baadhi ya Wanawake wafanyakazi wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) katika picha na watoto wanaolelewa katika kituo cha Yatima Group Trust Fund kilichopo Mbagala Chamanzi jijini Dar es salaam katika kuadhimisha siku ya Wanawake duniani.
PICHA NA NIC
…………………………………………………………………
Na Mwandishi wetu kutoka NIC
WANAWAKE watumishi wa Shirika la Bima la Taifa (NIC) wameaswa kuwa chachu ya maendeleo kwa kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili kuleta ushindani katika kuinua uchumi wa mwanamke mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Bima la Taifa Dkt. Elirehema Doriye wakati wa maadhimisho ya siku ya Wanawake Duniani yaliyofanyika kitaasisi katika ukumbi wa Makao Makuu ya Shirika hilo jijini Dar es salaam.
“Kaulimbiu ya mwaka huu ya maadhimisho haya inawapa nguvu wanawake kwenye kuleta maendeleo yenu binafsi, Shirika, jamii inayowazunguka na Taifa kwa jumla hasa katika kuimarisha Uchumi wa kati kuelekea uchumi wa juu”, alisema Dkt. Doriye.
Aidha Dkt. Doriye amesema kuwa kutokana na uwajibikaji wa wanawake katika Shirika hilo Bodi ya Wakurugenzi inafikiri kuongeza idadi ya viongozi wanawake mpaka kufikia asilimia 30 kwa maslahi ya mwanamke na taifa.
“Kutokana na ufanisi na uchapaji kazi wenu kama wanawake Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Shirika imefikiria kuongeza idadi ya viongozi wanawake mpaka kufikia asilimia 30 ili kuendelea kuchochea maendeleo ya Shirika letu”, amesisitiza Dkt. Doriye.
Katika kuadhimisha siku ya wanawake Duniani Wanawake wa NIC walitoa msaada wa fedha na vitu mbalimbali katika kituo cha kulelea watoto yatima cha Yatima Group Trust Fund kilichopo Mbagala Chamanzi jijini Dar es salaam kwa ajili ya kuwasaidia katika maisha yao ya kila siku.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mahitaji hayo katika kituo hicho Meneja Rasilimali watu wa wa Shirika la Bima la Taifa Bi. Veneranda B. Mpaze amesema kuwa wanawake wa NIC wameamua kufanya hivyo kwa kuwa ni sehemu mojawapo ya kurudisha kwa jamii.
“Katika kusheherekea siku ya wanawake Duniani sisi kama wanawake na wafanyakazi kutoka NIC tumeona ni vema kuja kujumuika na watoto wa kituo hiki kwa kuwapatia mahitaji mbalimbali ikiwemo, vyakula, vinywaji, sabuni za kuogea na za kufulia, mafuta ya kupaka pamoja na fedha”, amesema Bi. Mpaze.
Siku ya Wanawake Duniani huadhimishwa Machi 8 kila mwaka na kwa mwaka huu kitaifa imeadhimishwa Mlimani City jijini Dar es salaam.