Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabula akimkabidhi Bibi Maria Makasa Leseni yake ya Makazi wakati wa utowaji wa Leseni za Makazi kwa wakazi wa Mtaa wa Mabatini jiji Mwanza. Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabula (katikati waliokaa) akiwa pamoja na wakazi wa mtaa wa Mabatini jiji Mwanza waliopewa Leseni zao za Makazi.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabula akiwatangazia wakazi wa mtaa wa Mabatini jiji Mwanza mpango wa kutambua kila kipande cha ardhi na kutoa Leseni zao za Makazi.
Wakazi wa Mabatini jiji Mwanza waliohudhuria katika mkutano wa Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Dkt. Angeline Mabula wakati akiwatangazia wakazi wa mtaa wa Mabatini jiji Mwanza mpango wa kutambua kila kipande cha ardhi na kutoa Leseni zao za Makazi.
Na. Hassan Mabuye, Mwanza
Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imeanza kutekeleza mradi wa utambuzi wa kila kipande cha ardhi kwa ajili ya kupanga, kupima na kumilikisha vipande vya ardhi kwa kutoa leseni za makazi ndani ya siku 14.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo wa utambuzi na utoaji wa leseni za makazi katika viwanja vya shule ya msingi Mabatini wilaya ya Nyamagana Naibu Waziri wa Ardhi Mhe. Dkt. Angeline Mabula amesema kuwa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Mhe Dkt John Magufuli kupitia Wizara ya Ardhi imekusudiwa kuwatambua wananchi wote wanaoishi katika makazi ambayo hayajapangwa hivyo kuwapimia na kuwamilikisha ardhi yao.
Amesema lengo la mradi huu ni kuondokana na changamoto za kukosa miliki ya ardhi kisheria ikiwemo kuendeleza maeneo yao huku akiwasisitiza wananchi hao kuhakikisha wanalipa kodi ya pango la ardhi mara baada ya kukabidhiwa leseni hizo za makazi.
Aidha Naibu Waziri Dkt Mabula akawaasa wananchi hao kuhakikisha wanaendeleza miliki zao kwa kufuata sheria na taratibu za mipango miji pamoja na kulipa kodi ya pango la ardhi kwa wakati.
“Usipolipa kodi ya ardhi utaletewa Ilani ulipe na ukiendelea kukaidi utapelekwa katika baraza la ardhi ulipe, ikifika miezi sita hujalipa sheria inamtaka afisa ardhi mteule afute miliki yako bila hata kukwambia” Alisema Dkt. Mabula.
Kwa upande wake Kamishina wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mwanza Bwana Eliah Kamihanda amefafanua kuwa mradi huu ujulikanao kwa jina la ‘fit for purpose’ una lengo la kutambua vipande vya ardhi vilivyoendelezwa bila kufuata sheria na taratibu za mipango miji (makazi holela).
Kamihanda meongeza kuwa vipande vya ardhi 5,957 vinatarajia kutambuliwa na kumilikishwa kupitia utoaji wa leseni za makazi kwa mkoa wa Mwanza pekee, Wakianzia kata ya Mabatini huku tangu kuanza kwake mwezi januari mwaka huu kwa kata hiyo vipande vya ardhi 111 vimeshatambuliwa na kutolewa leseni za makazi kwa wamiliki wake
Nae mratibu wa mpango huo kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Godfrey Machabe akaongeza kuwa mpango wa kupanga, kupima na kumilikisha vipande vya ardhi kwa kutoa leseni za makazi kwa kuanzia unatekelezwa katika mikoa miwili nchi nzima ikiwemo Mwanza na Arusha hivyo kuwataka wananchi kutumia vizuri fursa hiyo ili kupata umiliki wa kisheria kwa vipande vya ardhi wanavyovimiliki
Moja ya wananchi walionufaika na mradi huo Bwana Yona Fumi Ng’wenhelwa mkazi wa kata ya Mabatini akaishukuru Serikali kupitia wizara ya ardhi kwa kuendesha zoezi hilo kwani limemsaidia kutatua kero ya kukosa Mali isiyohamishika kisheria pindi anapotakiwa kumdhamini ndugu yake au kukopa katika taasisi za fedha sambamba na kuridhishwa na kasi ya maandalizi na utoaji wa leseni hizo kwani umetumika muda mfupi mpaka kuipata leseni yake ya makazi.