*************************************
NJOMBE
Licha ya Kasi ya ukuaji na maendeleo ya Sayansi na teknolojia duniani kote kutajwa kuwa na faida na hasara katika jamii ,wilayani Makete mkoani Njombe wazaliwa waishio ndani na Nje ya kata ya Lupila wakiongozwa na katibu mkuu wa wizara ya maji mhandisi Antony Sanga wametumia kundi suguzi(Whatsapp Group) kupeana elimu,kuhamasishana na kuchangisha fedha kiasi cha mil 2 na elfu 60 na kisha kutoa zawadi kwa uongozi wa shule ya sekondari Lupila kwa kufanya vizuri katika mtihani wa kidato cha 4 ,2021
Katika matokeo hayo shule hiyo ambayo imepokea kidato cha 5 kwa mara ya kwanza mwaka huu ,imefanikiwa kutokomeza zero huku ikiwa wanafunzi 4 waliopata daraja la kwanza na kuweka historia kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake.
Akizungumza wakati akikabidhi motisha hiyo katibu mkuu wa wizara ya maji mhandisi Antony Sanga amesema kitendo kilichofanywa na uongozi na wanafunzi wa shule hiyo kimewatoa kimasomaso na kuandika historia mpya wilayani Makete na kwamba kwa kufanya hivyo kutaongeza ari kwa wanafunzi na walimu kuendelea kuweka jitihada zaidi za kufanya vizuri.
Aidha Sanga amesema mapema baada ya kupata taarifa za shule ya sekondari Lupila kufanya vizuri katika matokeo ya kidato cha nne 2021 kupitia kundi la wazawa wa kata hiyo waishio ndani na nje walianza kuchangishana fedha ili kwenda kuwapa hongera na motisha walimu na wanafunzi.
“Tumechangishana fedha na kupata mil 1.7 na kisha kupitia msafara huu wameongeza laki 3 na elfu 50 akiwemo Dc wa Makete na mbunge na kufanya zaidi ya mil 2 ambazo nitazikabidhi hapaleo kwa walimu”alisema mhandisi Sanga.
Mbali na kuwapa motisha walimu ,Katibu mkuu pia ametoa mil 1 kwa wanafunzi shuleni hapo ili wabadirishiwe chakula na kinywaji ili kuendelea kufanya vizuri katika mitihani ijayo.
Mdau mwingine wa elimu ambaye ni mzawa wa kata ya Lupila ni Eliot Ndelwa ambaye nae ametekeleza ahadi yake aliyotoa mwaka jana katika mahafali yakidato cha kwanza ya kutoa kununua laki 2 kila daraja la kwanza shuleni hapo na kutoa mbuzi mmoja kwa walimu ,ambapo ametoa laki nane kwa wanafunzi wanne waliopata daraja la kwanza na kuahidi kuendelea kufanya hivyo kadili matokeo mazuri yatakavyopatikana.
Awali wakati wa makabidhiano ya fedha hizo mkuu wa wilaya ya Makete Veronica Kessy ambaye pia ametoa mchango wake shuleni hapo ametoa onyo na kuahidi kuwashughulikia walimu wanaoingia katika mahusiano ya kimapenzi na watoto wa shule na kisha kuwapoteza katika mwelekeo wao
Kufuatia motisha hiyo Abukasa Ngwale ambaye ni mkuu wa shule ya sekondari Lupila na Lulu Ismael ambaye ni mwanafunzi wanaeleza siri ya mafanikio yao na changamoto zinazokwamisha jitihada zao za kufikia malengo waliojiwekea kuwa ni miundombinu duni ya elimu zikiwemo nyumba za walimu,madarasa,umeme na jengo la chakula na kwamba endapo wataboreshewa watafanya vizuri zaidi.