****************************************
Jamii imetakiwa kulinda, kutunza na kutumia vizuri miundombinu ya michezo ikiwemo viwanja ili kutoa fursa kwa vijana kutumia miundombinu hiyo kwaajili ya kukuza vipaji vyao, kupata ajira na kuimarisha afya zao dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza
Rai hiyo imetolewa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa zoezi la kukabidhi vifaa mbalimbali vya michezo ikiwemo mipira kwa vilabu vya mchezo wa mpira wa kikapu, mpira wa pete, mpira wa miguu na mpira wa mkono vilivyopo mkoa wa Mwanza iliyotolewa na taasisi isiyo ya kiserikali ya Mwanza Charity ikishirikiana na manispaa ya Ilemela katika viwanja vya shule ya msingi Sabasaba ambapo amewataka wananchi kuwa walinzi wa miundombinu ya michezo iliyojengwa katika eneo hilo ikiwemo viwanja vya kisasa baada ya malalamiko juu ya uwepo wa baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waadirifu wanaotumia eneo hilo kuchimba mashimo yanayoharibu viwanja hivyo
‘.. Nitoe rai kwa mara nyengine viwanja hivi tuvitunze na tuvitumie kama ambavyo inastahili kutumika, Na nimuombe mkurugenzi kumetokea changamoto kwa wenzetu wa mpira wa miguu kuna wafanya biashara siku ya jumapili wanaingia katikati ya uwanja na wanachimba, Tukileta vifusi kwaajili ya kusawazisha hao wanavihamisha hili halikubariki …’ Alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula ameahidi kushirikiana na Serikali ili kumaliza changamoto zinazojitokeza bandarini pindi wadau hao wa maendeleo wanapoingiza vifaa vya michezo kutoka nje ya nchi huku akiwataka wananchi wa Ilemela kujivunia umaarufu wa wilaya hiyo katika kuzalisha na kukuza vipaji vya wachezaji tegemeo kwa vilabu vikubwa na taifa kwa ujumla
Kwa upande wake mratibu wa taasisi ya Mwanza Charity Ndugu Rogasian Kaijage mbali na kumshukuru mbunge huyo kwa ushirikiano anaoutoa akaongeza kuwa taasisi hiyo inakusudia kugawa mipira elfu ishirini na tano kwa vilabu vya wilaya zote zilizopo ndani ya mkoa wa Mwanza huku Ilemela pekee itakabidhiwa mipira elfu kumi kabla ya kuja na mpango wa nchi nzima sambamba na kuendelea na mkakati wa ujenzi wa viwanja vya michezo maeneo mbalimbali
Afisa Michezo wa manispaa ya Ilemela Mwalimu Bahati Kizito Sosho akavitaka vilabu vilivyopokea mipira hiyo kuhakikisha wanaitunza na kuitumia vizuri kwa lengo lililokusudiwa huku akiahidi kushirikiana na wadau katika kukuza sekta ya michezo ndani ya wilaya hiyo.
Nae mmoja kati ya wanufaika wa mipira iliyotolewa kutoka klabu ya mpira wa miguu ya Yosa iliyopo kata ya Igombe Hamza J. Hamza akashukuru kwa vifaa hivyo kwani vitawasaidia katika mazoezi ya kila siku na kufanya vizuri katika mashindano mbalimbali yatakayojitokeza huku akiahidi kuvitunza vifaa hivyo.