Kikundi cha wanawake kutoka Taasisi binafsi ya kuwezesha Sekta ya Kilimo Tanzania (PASS) wakimsikiliza mama ambaye mtoto wake amelazwa katika wodi ya watoto wenye magonjwa ya moyo walipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa ajili ya kulipia gharama za upasuaji kwa watoto wawili, kuwakatia kadi za bima watoto kumi pamoja na kutoa mahitaji madogo madogo kwa watoto waliolazwa katika wodi hiyo leo Jijini Dar es Salaam.
Mama ambaye mtoto wake anasumbuliwa na maradhi ya moyo Anganile Mwaisaka akitoa machozi ya furaha baada ya kikundi cha wanawake kutoka Taasisi binafsi ya kuwezesha Sekta ya Kilimo Tanzania (PASS) kutoa msaada wa Tshs. 2,000,000 ambazo ni gharama za kufanyiwa upasuaji wa moyo kwa mtoto huyo leo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Jijini Dar es Salaam.
Kikundi cha wanawake kutoka Taasisi binafsi ya Kuwezesha Sekta ya Kilimo Tanzania (PASS) wakikabidhi zawadi za Huggies diapers, sabuni za unga za kufulia, dawa za meno, miswaki na mafuta ya kupaka mwilini kwa ajili ya matumizi ya watoto waliolazwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kiwete (JKCI) ikiwa ni katika kuadhimisha siku ya wanawake Duniani.
Meneja Rasilimali watu na Utawala kutoka Taasisi binafsi ya kuwezesha Sekta ya Kilimo Tanzania (PASS) Elita Naimani pamoja na Mkuu wa Idara ya Watoto wenye magonjwa ya moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Sulende Kubhoja wakipitia majina ya watoto watakaosaidiwa gharama za upasuaji pamoja na kukatiwa kadi za bima ya afya baada ya wanawake kutoka taasisi hiyo kukabidhi kiasi cha Tsh. 4,540,000 kwa ajili ya kuwasaidia watoto wanaotoka katika familia zenye uwezo mdogo kiuchumi . Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
Picha na: JKCI
*************************************
Wazazi na walezi nchini wameshauriwa kuwapeleka watoto wao katika vituo vya afya kwa ajili ya uchunguzi na matibabu stahiki pindi watakapoonesha viashiria vyovyote vya ugonjwa.
Wito huo umetolewa leo na kiongozi wa kikundi cha wanawake kutoka Taasisi binafsi ya kuwezesha sekta ya kilimo Tanzania (Private Agricultural Sector Support-PASS) Elita Naimani walipotembelea Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) leo kwa ajili ya kuchangia gharama za matibabu kwa watoto wanaotibiwa katika Taasisi hiyo.
Elita Naimani ambaye pia ni Meneja Rasilimali watu na Utawala wa PASS alisema katika kuadhimisha siku ya wanawake Duniani wameona ni vyema watembelee watoto wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo ili wawajulie hali pamoja na kuwatia moyo mama zao wanaowauguza.
Alisema baada ya kuwatembelea watoto hao wameelezwa na wataalamu kuna baadhi yao wanasumbuliwa na maradhi ya moyo yanayotokana na bakteria wanaoshambulia valvu za moyo (Rheumatic Heart Diseases).
“Tumeambiwa na daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto kuwa maradhi haya yanatokana na mtoto kuumwa homa ya mafindofindo (tonsillitis) kama mtoto hatapata matibabu sahihi au hatamaliza dozi bakteria hao watashambulia valvu za moyo na hivyo mtoto kuumwa maradhi hayo”,.
“Hiki kitu kimenishtua sana kwani ni mara nyingi mtoto akiumwa unampa dawa ya maumivu pasipo kumpeleka hospitali. Ninawaomba wazazi wenzangu tuache tabia hii ukiona mwanao hayuko sawa Kiafya mpeleke hospitali kwa ajili ya matibabu na akipewa dawa hakikisha anakunywa kwa wakati na kumaliza dozi yote”, alisisitiza Elita.
Aidha katika kuchangia kwao gharama za matibabu ya watoto hao alisema waliona waiunge mkono kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya wanawake Duniani inayosema wanawake katika uongozi , chachu kufikia Dunia yenye usawa kwa kutimiza ndoto za watoto kwa kuwachangia gharama za upasuaji, kuwakatia bima za afya pamoja na kuwapatia mahitaji yao ya kila siku wawapo wodini.
Elita alisema, “Watoto hawa pamoja na kuwa wanapitia katika changamoto za ugonjwa wana ndoto zao kama ilivyo kwa watoto wengine hivyo basi tumekuja kuwasaidia kutimiza ndoto hizo kwa kuwachangia gharama za matibabu ili wakipona waendelee na maisha yao ikiwemo kusoma kama ilivyo kwa watoto wengine”,.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI Prof. Mohamed Janabi alikishukuru kikundi hicho cha wanawake kwa moyo wao wa upendo waliouonesha kwa watoto wanaotoka katika familia zisizo na uwezo kiuchumi kwa kuwachangia gharama za matibabu.
Prof. Janabi alisema matatizo makubwa ya moyo kwa watoto wanaotibiwa katika Taasisi hiyo ni matundu, mishipa ya damu ya moyo kutokukaa vizuri (Congenital Heart Diseases) pamoja na maradhi ya moyo yanayotokana na bakteria wanaoshambulia valvu za moyo (Rheumatic Heart Diseases).
“Asilimia kubwa ya wagonjwa wetu wanatoka katika familia zenye uwezo mdogo kiuchumi na hivyo kushindwa kulipia gharama za matibabu. Tunawashukuru kwa mchango wenu ambao utaokoa maisha ya watoto hawa na kuwarudishia tabasamu kama ilivyo kwa watoto wengine”, alisema Prof. Janabi.
Akizungumza kwa niaba ya kinamama ambao watoto wao wamelazwa katika wodi hiyo Anganile Mwaisaka aliwashukuru wanawake hao kutoka PASS kwa kulipia gharama za upasuaji wa moyo kwa watoto, kuwalipia bima za afya pamoja na kuwapatia zawadi mbalimbali.
Kikundi hicho kimetoa shilingi milioni nne kwa ajili ya upasuaji wa moyo kwa watoto wawili, Tshs. 540,000/= kwa ajili ya kulipia kadi kumi za bima ya afya kwa ajili ya watoto na kutoa zawadi za Huggies diapers, sabuni za unga za kufulia, dawa za meno, miswaki , mafuta ya kupaka mwilini kwajili ya matumizi ya watoto waliolazwa katika wodi hiyo.