***********************************
Na Mwandishi wetu
Dar es Salaam. Taasisi ya huduma za kifedha ya Faidika imetenga zaidi ya Shilingi billion 50 kwa ajili ya kuwakopesha wafanyakazi wa serikali na Taasisi zilizothibitishwa kwa mwaka 2021.
Mkurugenzi Mkuu wa Faidika, Bw. Baraka Munisi alisema kuwa mikopo hiyo inatolewa ndani ya siku tatu endapo mkopaji atatimiza masharti yaliyowekwa.
Masharti hayo kwa mujibu wa Bw Munisi ni kitambulisho cha kazi, stakabadhi moja ya mshahara wa mwezi uliotangulia , taarifa ya akaunti ya benki kuanzia miezi miwili na kuendelea na picha moja ya pasipoti.
Bw Munisi alifafanua kuwa wameamua kutenga kiasi hicho kikubwa cha fedha kwa ajili ya kuboresha maisha ya Watanzania.
Alisema kuwa mikopo hiyo utolewa kuanza shilling 200,000 hadi Shilling milioni 70 na urejeshaji wake unaanzia miezi sita (6) hadi 84.
“Pamoja na changamoto za miundo mbinu kwenye taasisi nyingi za fedha, Faidika inaamini kuwa kila mtu anastahili kupata huduma ya kifedha ndio maana tumepanua wigo kupitia mifumo ya kisasa zaidi ya teknolojia ili kuwafikia watanzania wote kwa lengo la kuboresha maisha yao,” alisema Bw. Munisi.
Aliendelea kwa kusema kuwa, Faidika inatoa mkopo wa nyongeza kwa wateja wake (top-up) pamoja na kununua mikopo kutoka taasisi zingine za kifedha na mabenki (loan takeover/buyback) na kutoa mkopo mpya kwa riba nafuu ambayo ni asilimia tatu (3).
“Faidika inaendelea kuwawezesha watanzania ili waweze kuboresha maisha katika sekta mbalimbali ikiwa pamoja na elimu, afya na kilimo. Mbali ya faida ya punguzo la riba, pia mkopaji atafutiwa mikopo yake endapo atafariki na huku taasisi yetu ikitoa rambirambi hadi kufikia sh 200,000.
Alisema kuwa Faidika imedhamiria kuboresha zaidi maisha ya watanzania kwa mwaka 2021 na miaka inayokuja.
“Tunawaomba wananchi kuchangamkia huduma hii ambayo ni ya kipekee na rahisi,” alisisitiza Bw. Munisi.