Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Saimon Anange pamoja na viongozi wa Halmashauri ya Mji Kasulu wakiwa wamekalia moja ya dawati lililotolewa na wazazi
Sehemu ya madawati 140 yaliyotokana na michango ya wazazi katika Shule ya Msingi ya Kidyama yaliyopokelewa na Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia shuleni hapo
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako, Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Saimon Anange na viongozi wa Halmashauri ya Mji Kasulu kwa pamoja wakikata utepe kuashiria kupokea rasmi madawati 140 yaliyotolewa na wazazi kwa ajili ya shule ya Msingi Kidyama.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wazazi waliojitolea kununua madawati 140 kwa ajili ya Shule ya Msingi Kidyama.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Kidyama wakishuhudia hafla ya upokeaji wa madawati 140 kutoka kwa wazazi kwa ajili ya shule yao. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Joyce Ndalichako na Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Saimon Anange wakiwasili katika Shule ya Msingi Kidyama kwa ajili ya kupokea madawati 140 yaliyopatikana kutokana na mchango wa wazazi.
************************************
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako amewataka wazazi na walezi kushirikiana na shule wanazosoma watoto wao ili kutatua changamoto ndogondogo zinazokabili shule hizi ili kuboresha mazingira ya usomaji kwa watoto hao.
Profesa Ndalichako amesema hayo mjini Kasulu alipokuwa akipokea madawati 140 katika Shule ya Msingi Kidyama yaliyotengenezwa na wazazi na walezi wenye watoto katika shule hiyo kwa hiari.
Waziri Ndalichako amewapongeza wazazi hao kwa juhudi zao katika kushirikiana na Serikali kuboresha mazingira ya ujifunzaji katika shule hiyo ili watoto wao waweze kusoma kwenye mazingira yaliyo bora.
“Sijapata kuona jambo kama hili, nawapongeza sana, nawashukuru kwa ushirikiano katika kuleta maendeleo na mmeonyesha ni kwa namna gani mnawapenda na kuwajali watoto wenu,” amesema Profesa Ndalichako.
Waziri huyo amesema ni vyema wazazi kote nchini wakashirikiana na shule kutatua changamoto ambazo zipo ndani ya uwezo wao ili kuwezesha watoto kusoma katika mazingira bora na rafiki.
Mkuu wa Wilaya ya Kasulu, Kanali Simon Anange amesema wazazi hao wameonyesha mfano bora wa ushirikiano katika kulea na kuwapatia elimu iliyo bora.
“Niwapongeze tu wazazi kwa kutengeneza madawati hayo 140 ambayo yatawezesha watoto kusoma katika mazingira mazuri, hii italeta chachu ya kujitoa kwa wananchi katika maeneo mengine,” amesema Kanali Anange.
Naye Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kidyama, Filbert Mlamke amemwambia Waziri wa Elimu kuwa shule hiyo ilikuwa na upungufu wa madawati 240 uliotokana na uandikishaji mkubwa wa watoto mwaka 2021.
Amesema baada ya upungufu huo, shule iliwashirikisha wazazi na kwa pamoja walikubaliana kila wazazi wanne watengeneze dawati moja na kulikabidhi shuleni na mpaka sasa wameshapokea madawati 140 na kufanya upungufu kuwa madawati 100.
Katika kuunga mkono juhudi za wazazi hao Waziri Ndalichako amechangia madawati 50.