Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wananchi, baada ya kukagua ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), inayojengwa na Kampuni ya Yapi Markezi, wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa kipande cha Ihumwa- Igandu ikiwa ni sehemu ya pili ya mradi huo, kutoka Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma, Machi 3, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), inayojengwa na Kampuni ya Yapi Markezi, wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa kipande cha Ihumwa- Igandu ikiwa ni sehemu ya pili ya mradi huo, kutoka Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma, Machi 3, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa kuhusu ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), inayojengwa na Kampuni ya Yapi Markezi, wakati alipokagua maendeleo ya ujenzi wa kipande cha Ihumwa- Igandu ikiwa ni sehemu ya pili ya mradi huo, kutoka Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma, Machi 3, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
********************************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameamua kuboresha miundombinu mbalimbali ya usafiri nchini ikiwemo ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa (SGR) ili kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo.
Ameyasema hayo leo (Ijumaa, Machi 5, 2021) baada ya kukagua maendeleo ya sehemu ya kipande cha pili cha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa cha kutoka Morogoro hadi Makutupora mkoani Dodoma.
Waziri Mkuu ambaye amekagua kipande cha kutoka Ihumwa hadi Igandu amesema ameridhishwa na kazi nzuri inayoendelea kufanywa na amewataka wananchi wajiandae kutumia reli hiyo ambayo inajengwa kwa ajili yao.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaongeza ufanisi wa usafirishaji wa abiria na mizigo kwa kupunguza muda wa safari, mfano kutoka Dar es Salaam – Dodoma muda utakuwa saa tatu badala ya saa nane za sasa.
Waziri Mkuu amewataka Watanzania waliopata kazi katika mradi huo wafanye kazi kwa uaminifu na weledi wa hali ya juu ili kuudhihirishia ulimwengu kwamba Watanzania wanaajirika. “Endeleeni kuchapakazi nyinyi ni mabalozi mtakaowawezesha wengine kupata ajira.”
Amewataka Watanzania wahakikishe wanazielewa vizuri shughuli wanazozifanya katika mradi huo ili baadaye waweze kuisimamia wenyewe reli hii ikiwa ni pamoja na kufanya ukarabati. “Tumieni ujenzi wa mradi huu kama sehemu ya kupata utaalamu.”
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Bw. Masanja Kadogosa amesema ujenzi wa kipande cha pili cha mradi wa ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Morogoro hadi Makutupora umefikia asilimia 56.1 na unatarajiwa kukamilika Februari, mwakani.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutashusha gharama za usafirishaji mizigo kati ya asilimia 30 mpaka 40 na kuifanya bandari ya Dar es salaam kuhimili ushindani. Kipande cha kutoka Morogoro – Makutupora chenye urefu wa kilomita 422 kinajengwa na Kampuni ya Yapi Merkezi kutoka nchi ya Uturuki kwa gharama ya shilingi bilioni 4.4.
“Reli hii itachochea mapinduzi ya kiuchumi kwa kanda nzima ya Afrika Mashariki na Kati hususani nchi zisizopakana na Bahari, hivyo kuchangia katika kukuza uchumi wa Taifa. Pia mradi huu utachochea uanzishwaji wa viwanda katika maeneo mengine ya nchi kwa kuwa utoa uhakika wa usafirishaji wa mali ghafi na bidhaa.”
Mkurugenzi huyo amesema mpaka kufika tarehe 01 Machi, 2021 mradi huu ulikuwa na wafanyakazi 8,014, ambapo 6,472 sawa na asilimia 81% ni Watanzania na 1,542 sawa na asilimia 19% ni raia wa kigeni na kwamba TRC imeendelea kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wataalamu wake mbalimbali, ambapo kwa sasa zaidi ya wataalamu 40 wanashiriki moja kwa moja kwenye ujenzi wa mradi wa SGR.