Mtunza kumbukumbu za afya kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Nuru Muhidini akimjazia fomu kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya ya moyo mkazi wa Mbagala wakati wataalam wa afya wanawake wa Taasisi hiyo walipokuwa wakitoa huduma ya vipimo hivyo bila malipo leo kwenye Viwanja wa Mbagala Zakheem katika kuadhimisha siku ya Wanawaje Duniani.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Hildergard Karau akimpima shinikizo la damu makazi wa Mbagala aliyefika katika viwanja vya Mbagala Zakheem leo kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo uliofanywa na wataalam wa afya wanawake wa JKCI katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani.
Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Getrude Yombo akimpima wingi wa sukari mwilini mkazi wa Mbagala aliyefika katika viwanja vya Mbagala Zakheem kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo uliofanywa na wataalam wa afya wanawake wa JKCI kwa muda wa siku mbili wakati wa kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani.
Daktari bingwa wa magonjwa ya Moyo wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Honoratha Maucky akimpima mapigo ya moyo mkazi wa Mbagala aliyefika katika viwanja vya Mbagala Zakheem kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo uliofanywa na wataalam wa afya wanawake wa taasisi hiyo jana kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani.
Afisa Lishe wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Husna Faraji akitoa ushauri kuhusu lishe bora kwa mkazi wa Mbagala aliyefika katika viwanja vya Mbagala Zakheem kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo uliofanywa na wataalam wa afya wanawake wa Taasisi hiyo Jana katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimpa ushauri wa umuhimu wa kuhudhuria kliniki ya magonjwa ya moyo Mkazi wa Mbagala aliyefika katika viwanja vya Mbagala Zakheem kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo uliofanywa na wataalam wa afya wanawake wa Taasisi hiyo Jana katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akizungumza na wakazi wa Mbagala waliofika katika viwanja vya Mbagala Zakheem kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo uliofanywa na wataalam wa afya wanawake wa JKCI Jana katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akimuonyesha Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu Mhe. Shabani Abubakari baadhi ya dawa zitakazotolewa kwa wakazi wa mbagala watakaukutwa na matatizo ya magonjwa ya moyo wakati wa upimaji wa afya ya moyo kwa wakazi wa Mbagala uliofanywa na wataalam wa Afya wanawake kutoka JKCI jana kwenye viwanja vya Mbagala Zakheem katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe. Godwin Gondwe akizungumza na wakazi wa Mbagala waliofika katika viwanja vya Mbagala Zakheem kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi wa afya ya moyo uliofanywa na wataalam wa afya wanawake wa JKCI Jana katika kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani.
Diwani wa Kata ya Mbagala Kuu Mhe. Shabani Abubakari akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wilaya ya Temeke walioungana na wataalam wa afya wanawake kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) jana katika Viwanja vya Mbagala Zakheem kwa ajili ya kuwafanyia uchunguzi wa magonjwa ya moyo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha siku ya Wanawake Duniani tarehe 8/3/2021. Wa pili kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa JCKI Prof. Mohamed Janabi
Picha na JKCI
****************************************
Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
Jumla ya watu 561 wamepimwa viashiria vya magonjwa ya moyo bila malipo katika upimaji maalum uliofanywa na wataalamu wa magonjwa ya moyo wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Upimaji huo ulioenda sambamba na utoaji wa matibabu pamoja na kupewa rufaa kwa wale waliokutwa na matatizo ulifanyika kwa muda wa siku mbili katika viwanja vya Mbagala Zakheem vilivyopo wilayani Temeke ulikuwa ni maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani tarehe 8, Machi 2021.
Akizungumza na waandishi wa habari hizi leo katika viwanja vya Mbagala Zakheem Mwenyekiti wa Wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji na wagonjwa mahututi Anjela Muhozya alisema katika upimaji huo pia walitoa elimu ya lishe bora kwa afya bora ya Moyo.
Dkt. Anjela alisema kati ya watu 561 waliowapima asilimia 80 walikutwa na shinikizo la juu la damu kati ya hawa asilimia 50 walikuwa wanajijua kuwa na tatizo lakini hawakuweza kuendelea na huduma za matibabu kutokana na sababu mbalimbali za maisha, asilimia 30 hawakuwa wanajijua kabisa kama wanatatizo hilo hawa walianzishiwa matibabu.
Waliokutwa na matatizo asilimia 40 waliweza kukamilisha huduma ya matibabu katika viwanja hivyo hii ikiwa ni pamoja na kupewa dawa na ushauri na asilimia 20 walipewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete na Hospitali ya Temeke.
“Kati ya watu tuliowapima asilimia 10 hawakuwa na tatizo lolote la kiafya ila uzito wao ulikuwa mkubwa kitu ambacho ni hatari kwa afya ya moyo. Hawa tumewapa ushauri wa kubadili mfumo wa maisha katika ulaji wao wa vyakula pamoja kufanya mazoezi mara kwa mara”, alisema Dkt. Anjela.
Mkuu wa wilaya ya Temeke Godwin Gondwe aliwashukuru wataalamu wa JKCI kwa moyo wao wa upendo wa kuwafikiria wananchi wanyonge na kwenda kuwapa huduma ya upimaji na matibabu ya moyo bila malipo yoyote yale.
“Ninawashukuru sana kwa upendo wenu wa kuwafuata wananchi wanyonge na kuwapa huduma ya matibabu ya kibingwa ya moyo kama tunavyofahamu matitabu haya yanagharama. Kwa kuwafuata kwenu wananchi hawa wameweza kuokoa fedha ambazo wangelipia hospitali na kwenda kuzitumia katika matumizi yao ya kila siku”.
“Pia Afisa Ustawi wa jamii ameweza kuwasikiliza watu wenye shida za kijamii na kuwapa maelekezo ya jinsi gani wataweza kufika JKCI na kupata matibabu. Hii itawasaidia kutoogopa kufika pale kwa ajili ya kutibiwa kwa kuwa hawana uwezo wa kulipia gharama za matibabu”.
Gondwe alisema wilaya yake itaendelea kushirikiana na JKCI katika kuhakikisha wananchi wanyonge wanafikiwa na wataalamu wa taasisi hiyo na kuwaomba wananchi wa Temeke kutumia fursa hiyo ya upimaji wa afya zao bila malipo.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi alisema amefika katika viwanja vya Mbagala Zakheem kwa ajili ya kuwaunga mkono wanawake wa Taasisi hiyo kwa kufanya upimaji kwa wananchi.
“Kama mnavyoona tunafanya upimaji kwa wanawake na wanaume na wale ambao wamekutwa na matatizo wameanzishiwa matibabu kwa kupewa dawa na wengine watakuja JKCI kwa ajili ya matibabu ya kibingwa”.
“Taasisi yetu itaendelea kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanafikiwa na huduma za matibabu ya kibingwa pamoja na kupata elimu ya magonjwa hayo ambayo siyo magonjwa ya kuambukiza na kama mtu atakuwa na uelewa nayo ataweza kuyaepuka”, alisisitiza Prof. Janabi.
Naye Musa Kitimla ambaye ni mkazi wa Mbagala Kibondemaji alisema alisikia katika redio kuna huduma za upimaji wa moyo ambao utafanyika kwa muda wa siku mbili katika viwanja vya Mbagala Zakheem akaona ni muhimu kufika hapo kwa ajili ya kupima afya yake.
“Ninamshukuru Mungu nimefika hapa na kupata huduma mbalimbali za kupima afya na majibu yangu yameonekana sina tatizo lolote lile. Nitaendelea kuichunga afya yangu ili iendelee kuwa salama. Ninawasihi wananchi wenzangu wakisikia mahali kuna upimaji wa aina hii waende kwani licha ya kupima afya zao watapata ushauri pia”, alisema Kitimla.
Katika upimaji huo wananchi walipimwa urefu, uzito, shinikizo la damu (BP), sukari, Virusi vya Ukimwi na kupewa ushauri wa lishe bora. Kwa wale waliokutwa na matatizo ya moyo wamepewa rufaa ya kwenda kutibiwa katika Taasisi hiyo na Hospitali ya Temeke ili waweze kufanyiwa uchunguzi zaidi na kupatiwa matibabu.