……………………………………………………………………………………
Mkuu wa mkoa wa Iringa Ally Happi amewataka wabunge wanaotokea mkoa wa Iringa kubeba ajenda ya barabara kama ajenda ya pamoja ili kuwavutia wawekezaji na kukuza uwekezaji kwa lengo la kuinua uchumi wa mkoa wa Iringa.
Akizungumza katika kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa wa Iringa Hapi amesema Wabunge ni kielelezo muhimu cha maendeleo ya mkoa na wao wana nafasi kubwa ya kuusemea Mkoa kupitia Bunge kwa hivyo amewataka Wabunge hao kwa pamoja kuzizungumzia barabara mbalimbali za kiuchumi zilzopo ndani ya mkoa wa Iringa ili kufungua fursa mbalimbali zilizopo.
Akitolea mfano Barabara ya Iringa kuelekea hifadhi ya Taifa ya Ruaha alisema ni barabara muhimu sana ya kiutalii kwa hivyo wakiunganisha nguvu na kusemea barabara hiyo itafungua kwa kiasi kikubwa fursa za uwekezaji na kuongeza uchumi wa mkoa wa Iringa na taifa kwa ujumla.
Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli imehakikisha barabara nyingi zinatengenezwa hivyo ni jukumu la wabunge kuhakikisha wanasemea miradi ya barabara ambayo mafungu yapo kuweza kutolewa kwa wakati kuweza kukamilisha miradi hiyo.
“Bila barabara hakuna uchumi,afya, elimu wala uwekezaji hivyo miundo mbinu bora huwezesha wawekezaji kuja na kuwekeza hivyo jukumu la wabunge wetu kuichukua kama ajenda na kuipeleka bungeni kwa lengo la kuhakikisha miundo mbinu hasa ya barabara inakamilika hasa zile za kimkakati katika kukuza uchumi.” Alisema
Aidha aliongeza kuwa mkakati wa uwekezaji hauna maana kama hakuna miundo mbinu na kutoa wito kwa Tanroads na Tarura kuhakikisha watatambua wajibu na dira ya mkoa wa Iringa na kuhakikisha barabara zinakamilika katika muda mwafaka na zenye viwango.
Kwa upande wao Wabunge hao wamepokea wazo hilo la ushirikiano na kwa pamoja wameahidi kuisimamia ajenda hiyo ya Barabara huku kila mmoja akieleza changamoto mbalimbali wanazokumbana nazo kutokana na miundombinu mibovu ya barabara katika Majimbo wanayoyawakilisha.
Naye Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Iringa Mhandisi, Daniel Kindole alisema kuwa kazi ya upembuzi yakinifu, usanifu wa kina na kuaandaa makabrasha ya zabuni kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami umekamilika kwa barabara ya Kutoka ipogolo Iringa mjini hadi Kilolo yenye km 33.61.
Mhandisi Kindole aliongeza kuwa kazi hiyo ilifanyika mwaka wa fedha 2008/2009 na kazi ya kuhuisha ilikamilika mwaka 2019 kilometa 33.61, na hadi tarehe 28 Februari, 2021 kiasi cha kilometa 8.62 zimejengwa kwa kiwango cha lami.
Hata hivyo, serikali kwa kutumia fedha za ndani inajenga jumla ya km 10 kwa gharama ya Zaidi ya shilingi bilioni 7.889/-, ambapo utekelezaji wake hadi 28/02/2021 ni asilimia 67.
Aidha kwa mwaka wa fedha 20202/2021 barabara hii imetengewa fedha kwa ajili ya ujenzi kwa kiwango cha lami kuanzia Kilolo hadi Idete km 33.39 wilayani Kilolo, na utekelezaji wake upo katika hatua ya manunuzi.
Aidha aliongeza kuwa TANROADS inatarajia kuanza ujenzi wa barabara ya mchepuo (bypass) wa mji wa Iringa kuanzia Kihesa Kilolo kupitia Chuo Kiuu cha Iringa (UOI) hadi Igumbulo barabara ya TANZAM.
Alisema kuwa wizara ya ujenzi kupitia TANROADS imekamilisha kazi ya usanifu wa kina wa barabara ya mchepuo wa Mji wa Iringa yenye urefu wa km 7.3 kuanzia Kihesa Kilolo kupitia UOI hadi Igumbilo kwenye barabara kuu ya TANZAM.
Kindole alikiambia kikao cha bodi cha barabara kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara ya Iringa-Dodoma (km 260) kwa kiwango cha lami kumepelekea kuongezeka kwa magari kwenye barabara hiyo na hivyo kusababisha msongamano mkubwa wa magari mjini Iringa.
Aliongeza kuwa zoezi la kulipa fidia wananchi walioathirika na ujenzi wa barabara hiyo limekamilika, fedha iliyolipwa kwa ajili ya fidia ni shilingi bilioni 4.62/- kwa mali zote zinazoathirika na mradi.
Hata hivyo, serikali kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ilitenga shilingi 950.000m/- kwa ajili ya ujenzi wa km 0.450 kutoka Igumbilo Stendi Kuu ya mabasi yaendayo mikoani kuelekea Chuo Kikuu cha Iringa (UOI) (Iringa bypass) kazi imekalika.
Ofisi ya meneja wa wakala wa barabara (TANROADS) mkoa wa Iringa inahudumia barabara zenye urefu wa km 1,218.5 ikijumilisha km 462.3 za barabara kuu na km 756.2 barabara za mkoa, ambapo mtandao wa barabara tajwa hapo juu unajumilisha barabra za lami km 426.5 na za changarawe/ udongo km 792.0.