…………………………………………………………………………………..
Na Damian Kunambi, Njombe
Viongozi wa dini pamoja na wazee wilayani Ludewa mkoani Njombe wamemtaka mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga kuhakikisha anafuatilia suala la kumalizia majengo ya nyumba za jeshi la polisi wilayani humo ambazo ujenzi wake umekwama kwa zaidi ya miaka 13 na kupelekea majengo hayo kuzungukwa na pori.
Wazee hao na viongozi wa dini wameyasema hayo katika vikao vilivyofanywa kwa nyakati tofauti na mbunge huyo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kusikiliza changamoto mbalimbali za wananchi zinazowakabili ili kuweza kuzitafutia ufumbuzi thabiti ikiwemo na kwenda kuyasemea bungeni.
Steven Kalinjila ni mwalimu mstaafu na Padri Andrew Hiluka ni katibu msaidizi wa kamati ya dini mbalimbali na uhusiano wilaya ya Ludewa wamesema kuwa ujenzi wa nyumba hizo umesimama kwa muda mrefu sana na zinaharibu sura ya wilaya hivyo wangependa zimaliziwe ili polisi waweze kuishi humo.
Steven Kalinjila aliongeza kuwa askari hao wanapoishi mitaani hupelekea kuzoeana na raia kitu ambacho endapo raia hao wanafanya makosa na kufikishwa kituoni kwa makosa mbalimbali hupelekea kesi kutochukuliwa kwa uzito kwakuwa ni watu waliozoeana.
“Tunaomba mbunge wetu ufuatilie suala hili kwa ukaribu sana na kuhakikisha nyumba hizi zinamaliziwa kwakuwa hatua zilizofikia ni kubwa kuliko zilizobaki, hii itawasaidia askari wetu kufanya kazi katika mazingira mazuri na yenye weledi zaidi”, Alisema Kalinjila.
Imeelezwa kuwa nyumba hizo zilianza kujengwa mwaka 2007 kipindi ambacho profesa Raphael Mwalyosi akiwa ni mbunge wa jimbo hilo ambapo alijenga nyumba hizo na kuishia kwenye linta na alipotoka madarakani mwaka 2010 aliingia marehemu Deo Filikunjombe ambaye naye alipaua na kupiga bati pamoja na lipu na toka hapo hazikufanyiwa tena ukarabati wowote mpaka sasa.
Akitolea majibu suala hilo mbunge wa jimbo hilo Joseph Kamonga amesema tayari ameshaanza kufuatilia katika hatua za awali ambapo kwa nyakati tofauti alikutana na Waziri wa mambo ya ndani pamoja na naibu wake na kuwaeleza juu ya majengo hayo ambapo waliahidi kushughulikia.
Amesema hataishia hapo ataendelea kufuatilia ili kuona linafanyiwa kazi kwani nyumba hizo zina umuhimu mkubwa sana kwa jeshi la polisi na endapo zitakamilika zitawasaidia kuishi kwa pamoja na kujenga mahusiano yaliyo mazuri kati yao.
“Nikweli polisi wetu wanapoishi mitaani hupunguza ufanisi wa kazi zao kwani endapo inatokea mwenyenyumba wake anafanya kosa itamuwia vigumu kumchukulia hatua kutokana na kuwepo na mgongano wa kimaslahi kati yao hivyo ni vyema askari hawa wakaishi eneo nje ya raia wa kawaida”, Alisema Kamonga
Sanjali na suala hilo la ujenzi wa nyumba za jeshi la polisi pia mwenyekiti wa baraza la ushauri la wazee Onesmo Haule aliwasilisha maoni ya jumla yaliyotolewa na wazee hao kuwa kuna haja ya kuboresha suala la uchumi wa wilaya hiyo kwa kuimarisha mazao ya kibiashara kwa maeneo mbalimbali kulingana na tabia ya ukanda husika.
Amesema kuwa wilaya hiyo ina tarafa tano ambapo kwa tarafa ya masasi wanapaswa kuboresha kilimo cha zao la korosho kuwa cha kisasa, tarafa ya Mawengi, Liganga na Mlangali kuimarishwe kilimo cha parachichi, kahawa, pareto pamoja na chai haya ni mazao ambayo yakisimamiwa vyema yatasaidia kukuza uchumi wa Ludewa.
Aliongeza kuwa kwa upande wa tarafa ya mwambao wazee hao wameshauri kuboreshwa kwa uvuvi na kuwasaidia wavuvi hao kupata nyenzo za kisasa ili ziwawezeshe kuingia ndani zaidi ya ziwa na kuvua samaki huku wakishauri pia kuanzishwa kwa kilimo cha zao la chikichi ili kupata mafuta ya mawese ambapo kwa ukanda huo itawasaidia kujiongezea kipato.
Huku Padri Andrew Hiluka ambaye ni katibu msaidizi wa kamati ya dini mbalimbali na uhusiano wilaya ya Ludewa aliwasilisha maoni yaliyojadiliwa kwa pamoja na viongozi hao wa dini kuwa wanaomba kuharakishwa kwa ujenzi wa daraja linalounganisha mkoa wa Ruvuma na wilaya ya Ludewa lililopo mto Luhuhu ili kuweza kufungua fursa mbalimbali za maendeleo pamoja na ujenzi wa chuo cha VETA katika kijiji cha Shaurimoyo kwakuwa vijana wanazagaa mitaani baada ya kumaliza elimu zao za msingi na sekondari kitu ambacho kingewasaida kupata ujuzi mbalimbali.
Akitanabaisha hayo mbunge huyo alisema amepokea maoni hayo huku akitolea majibu baadhi ya maoni tayari yameshaanza kufanyiwa kazi huku akisistiza kuyashughulikia mawazo mapya na ambayo yalikuwepo ili kuweza kuleta maendeleo katika jimbo lake.