Home Mchanganyiko MUHIMBILI YAFUNGA MASHINE ZA KUTOA TIBA MVUKE, WATAALAM KUZIFANYIA UTAFITI

MUHIMBILI YAFUNGA MASHINE ZA KUTOA TIBA MVUKE, WATAALAM KUZIFANYIA UTAFITI

0

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ufungwaji wa  mashine nne za kutoa dawa kwa njia ya mvuke (steam inhalation machines)

Mkurugenzi Mtendaji Hospitali ya Taifa Muhimbili Prof. Lawrence Museru akitoka kwenye mashine ya tiba  mvuke.

………………………………………..

Hospitali ya Taifa Muhimbili imefunga mashine nne za kutoa dawa kwa njia ya mvuke (steam inhalation machines) zilizotengenezwa nchini na Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) ili kusaidia wagonjwa kupata tiba ya mfumo wa upumuaji kwa njia ya mvuke (steam therapy) kwa kutumia dawa zilizoidhinishwa na Serikali.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Prof. Lawrence Museru amesema hatua hii ni kuunga mkono jitihada za Serikali katika kukabiliana na magonjwa yanayohusiana na mfumo wa upumuaji.
 
“Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ilielekeza kuimarishwa matumizi ya dawa za tiba asili na tiba mbadala kwa wagonjwa walioko hospitalini kama nyongeza (supplement) kwenye tiba za kibingwa wanazopewa. Katika kutekeleza hilo hospitali imekuja na utaratibu wa kuwaruhusu wagonjwa kwa hiari yao kutumia dawa za tiba asili za kunywa na mvuke (steam therapy) zilizoidhinishwa na Serikali sambamba na tiba za kibingwa wanazopewa,” amesema Prof. Museru.
 
Ameeleza kuwa hatua ya ufungwaji wa mashine hizo utakwenda sambamba na kutoa fursa kwa wataalamu wa Muhimbili kufanya utafiti kubaini ufanisi wa baadhi ya dawa zinazogunduliwa na baadhi ya wataalamu wa tiba asili nchini ili hatimaye kuja na majawabu.
 
“Katika hospitali zetu za Upanga na Mloganzila tuna madaktari wa aina mbalimbali takribani 400 ambao baadhi yao kupitia matumizi ya huduma hii ya tiba mvuke watafanya utafiti na kuwa katika nafasi ya kutuambia kama tiba hizi zinasaidia kwa kiasi gani, kwa kuwa ugonjwa huu wa Covid 19 ni mpya hakuna aliye na  majibu sahihi, kwa hiyo  ni muhimu kwamba hizi njia zinazojitokeza za kupambana na matatizo haya sisi tuliopo hapa tusizipuuzie bali tuzifanyie utafiti na kutoa majibu,” amesema Prof Museru
 
Amesema kuwa mashine tatu zimefungwa Upanga na moja imefungwa Mloganzila ambapo zitaanza kutumika rasmi tarehe 05 Machi, 2021 kwa utaratibu maalumu ambapo wagonjwa watakaoruhusiwa ni wale watakaokubali kwa hiari yao wenyewe na wale wanaoweza kutembea na kusimama wenyewe kwenye mashine kwa muda usiozidi dakika tano. Aidha Prof. Museru amesema kuwa  huduma iko wazi kwa wananchi watakaopenda kufika kuitumia atatakiwa kuchangia kiasi cha shilingi elfu 5.
 
Naye Mratibu wa Tiba Asili na Tiba Mbadala wa Mikoa na Wilaya kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Vumilia Liggyle amepongeza hatua ya Muhimbili kufunga mashine za kutoa tiba mvuke na ametoa wito kwa hospitali na taasisi nyingine nchini kuiga mfano wa huo ili kuendelea kupambana na magonjwa ya kuambukiza na yasiyo ya kuambukiza.