………………………………………………………………………….
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Mh.Josephat Maganga amewatoa hofu wakazi wa Wilaya hiyo juu ya upatikanaji wa huduma ya maji huku akisema kuwa Mamlaka ya maji safi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) inafanya jitihada kubwa kuhakikisha inaondoa tatizo la maji jijini humo.
Mh.Maganga ameyasema hayo hii leo mara baada ya kukagua na kujionea maendeleo ya visima vikubwa vinavyochimbwa katika eneo la Mzwakwe Bonde la Makutupola ambapo pamoja na mambo mengine ameonesha kuridhishwa na maendeleo yake hivyokuwapongeza DUWASA na kusema kwa sasa wananchi wakae mkao wa kula kwani visima hivyo vitakapokamilika vitatatua kwa kiasi kikubwa changamoto ya upatikanaji wa maji jijini Dodoma
”Kazi inayoendelea hapa haina ubishi kwamba itatutoa hapa tulipo na kutufikisha mahala ambapo tunastahili kuwepo,kwa kuwa kama maji yataongezeka hata usambazaji wa maji utaongezeka pia,nitoe wito kwa wananchi wakae mkao wa kula tu kupata maji”Alisema.
Aidha Maganga ametoa wito kwa wananchi kutokuiharibu miundombinu ya maji iliyowekwa na badala yake kuitunza
”Mimi kwa niaba ya Serikali ya Wilaya naipongeza Serikali kuu pia nawapongeza sana DUWASA chini ya Mkurugenzi wao kwa jitihada kubwa wanazozifanya,Nitoe wito tu kwa wananchi wote wa Dodoma tuwe walinzi wa vyanzo na miundombinu ya maji kwa sababu maji ni uhai”Alisema Maganga
Na kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA Mhandisi Aron Joseph amesema kutokana na ongezeko la watu Dodoma wanafanya jitihada kubwa kuhakikisha tatizo la maji linapungua
”Dhumuni la ziara hii ni kumfikisha Mkuu wa wilaya kuja kujionea maendeleo ya uchimbaji wa visima hivi ambavyo vinalenga kupunguza tatizo la maji katika jiji la Dodoma na nimhakikishie tu kwamba kazi inakwenda vizuri na itakamilika ndani ya muda”
”Maji tunayoyachimba hapa yanatoka chini ya Ardhi na chini ya Ardhi kuna miamba mbalimbali ikiwemo madini,chumvi na kadhalika,lakini sisi tuna vipimo na vipimo hatujaanzisha sisi DUWASA bali vipo vya nchi lakini pia vipo vya WHO kuhakikisha kwamba maji tunayoyasambaza yanakuwa na madini yanayo takiwa ambayo hayajazidi viwango vinavyo takiwa”
”Kumekuwa na suala la maji kuwa na chumvi ambalo watu wanazungumzia lakini niwahakikishie kuwa yako ndani ya kipimo ambacho hakina athari kwa matumizi ya binadamu kwa mujibu wa vipimo vya kitaifa”
”Uchimbaji wa visima hivi vitatu ambavyo tunavichimba tunategemea kupata maji yasiyopungua lita Milioni 21 hadi 28 inategemea na uwezo wa kisima kwa hiyo tuna upungufu wa Lita Milioni 37 kwa siku kama tutapata Maji Lita Milioni 21 mpaka 28 tutakuwa tumepunguza kwa kiasi kikubwa upungufu wa maji jijini Dodoma”Alisema Mhandisi Joseph
Kufuatia hatua hiyo inayochukuliwa na Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira jijini Dodoma wananchi wameaswa kuondoa hofu ya upungufu wa maji inayowakabili kwa hivi sasa kwani pindi visima hivyo vitakapokamilika imeelezwa kuwa vitapunguza adha hioyo kwa asilimia kubwa.