Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mwita Waitara (wakati) akizungumza na Watumishi wa Halmashauri ya Kigamboni Jijini Dar es Salaam (hawapo pichani).
Baadhi ya watumishi wa Kigamboni wakisikiliza kwa makini maelezo yanayotolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mwita Waitara (hayupo pichani)
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mwita Waitara akipanda mti baada ya kuwasiri katika kiwanda cha Lake Cement Limited Kigamboni Dar es Salaam.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Mwita Waitara akipokea maelezo kutoka kwa Biswajeet Malliki Operesheni meneja wa kiwanda cha Lake Cement Limited kilichopo Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mwita Waitara akizungumza na wafanyabiashara wa soko la Feri Kigamboni Jijini Dar es Salaam akiwa katika ziara ya kukagua mazingira ya soko.
***************************************
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Mwita Waitara amesema kwamba Kumekuwa na mazoea ya watu kutupa taka hovyo barabarani na kupelekea taka hizo kwenda kwenye mitaro na mifereji na kusababisha uchafuzi wa mazingira na mafuriko, hivyo Manispaa zote zinahitaji kuweka nguvu ya ziada katika kusimamia na kuhakikisha wale wote wanaotupa taka hovyo wanachukuliwa hatua za kisheria.
Ameyasema hayo alipokuwa katika ziara ya ukaguzi wa mazingira katika Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Ameeleza kuwa uchafuzi wa mazingira katika Jiji la Dar es Salaam uwe historia kwa sasa jiji linatakiwa kuwa safi kulingana na hadhi ya jiji kama vile Mhe. Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli alivyoweka nguvu kubwa katika miundombinu katika jiji hilo.
“Katika Mikoa iliyopendelewa na Mhe. Rais Dkt. John Magufuli kwa miundombinu ni Dar es Salaam hivyo tusikatishe tamaa juhudi zake katika kuendeleza jiji kuna haja ya kusimamia na kuhakikisha jiji linakuwa safi ili kutimiza adhma ya Mhe. Rais” Mhe. Waitara
Aidha ameleza kuwa utunzaji wa mazingira ni wajibu wa kila mmoja hivyo kuwe na mpango mahususi wa kuhifadhi na kutunza mazingira kwa kuhakikisha taka zote zinazozalishwa zinahifadhiwa vizuri na sio kuzitupa hovyo
“Kupata mafuriko katika jiji la Dar es Salaam ni dhahiri inaonyesha kuwa kunauzembe katika kusimamia taka zinazozalishwa na wakazi, hivyo nataka kukutana na wenyeviti wa mitaa, watendaji wa mitaa, madiwani, wabunge na watu wa mazingira kwenye kata kupata taarifa za kimkoa hususani za kimazingira namna walivyojipanga kusimamia mazingira katika Mkoa na mazingira yao kwa ujumla”
Mhe. Waitara katika ziara yake pia amekagua soko la Feri lililopo Manispaa ya Kigamboni pamoja na Kiwanda cha Saruji cha Lake Cement Limited kilichopo Kigamboni kujionea hali halisi ya kimazingira katika maeneo hayo. Akiwa katika Kiwanda cha Lake Cement Mhe. Waziri amesema kuwa mwanzoni kulikuwa na changamoto za vumbi na kelele katika kiwanda hiko lakini kwa asilimia kubwa wamezirekebisha hivyo waendelee kutunza Mazingira kwa manufaa ya Taifa na jamiii kwa ujumla
“kwa sasa kiwanda hakina shida lakini wajiwekee utaratibu wa kukagua mitambo yao mara kwa mara ili kuepuka uchafuzi wa mazingira. Nawapongeza kwa kuzingatia maelekezo waliyopewa na NEMC na wasirudie makosa tunataka viwanda vyote vinavyozalisha bidhaa kuzingatia sheria ili kuepuka malalamiko kwa wananchi na kuhakikisha mazingira yetu ni salama” alisema
Vile vile Mhe. Waitara amekagua soko la Feri kigamboni na kubaini changamoto kubwa katika ukusanyaji wa taka katika soko hilo na kupelekea wananchi kuchukizwa na uchafu katika soko hilo “Naagiza Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni kutenga sehemu ambayo itatumika kukusanyia taka ili kuepusha harufu na kusambaa kwa taka katika eneo la soko”
Naye Mkuu wa Idara ya Mazingira Juvenalis Mauna amekiri kuwepo kwa changamoto ya ukusanyaji wa taka ngumu Manispaa ya Kigamboni lakini Manispaa inajitahidi kuweka nguvu ya ziada katika kusimamia na kuhakikisha mazingira yanabaki kuwa safi na salama
“Mkakati wa Manispaa ni kuhakikisha taka zote zinazozalishwa zinahifadhiwa vizuri ili kuepuka kusambaa hovyo mitaani hivyo tumetengeneza matela tutahakikisha kila siku tela hilo linapita kukusanya taka ili kuepusha adha kwa wananchi lakini tunaomba wananchi wapokee jambo hilo na wao wawe wasafi ili kuepusha changamoto hizo.” alisema Mauna
Naibu Waziri Mwita Waitara leo yuko siku ya pili ya ziara yake katika Mkoa wa Dar es salaam akikagua masuala mbalimbali yanayohusu utunzaji na uhifadhi wa mazingira katika Mkoa huo.