………………………………………………………………………………….
Na Damian Kunambi, Njombe
Wananchi wa kata ya Kilondo tarafa ya Mwambao wilayani Ludewa mkoani Njombe wameiomba serikali kuwakamilishia mradi wa umeme ulionza kutekelezwa mwaka 2015 kupitia maporomoko ya maji ya mto Kilondo ambao uliishia njiani kutokana na changamoto mbalimbali ikiwemo kukosekana fedha za ujenzi wa mradi huo.
Alto Mwakila na Josephat Mwandesele ni miongoni mwa wananchi hao waliotoa maombi hayo mbele ya mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga pamoja na kamati ya siasa ya chama cha mapinduzi (CCM) wilayani humo walipofanya ziara katika katika tarafa ya mwambao ili kupokea changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi wa ukanda huo na kuzitafutia ufumbuzi.
wananchi hao wameiomba serikali kupitia mbunge huyo kuangalia mradi huo upya kwa kuwa ndio tegemeo lao la pekee kwa sasa katika ndoto za kupata nishati ili kuinua uchumi wa kata za tarafa hiyo uliodumaa kwa kukosa miundombinu ya nishati hiyo ya umeme.
“Wananchi bado tunashauku na huu mradi tunaiomba serikali iliangalie hili kwa jicho la huruma kwasababubu tunashida ya umeme tunatamani kuanzisha viwanda mbalimbali ikiwemo kusindika samaki lakini tunakwama kwasababu ya kukosa umeme”alisea Josephat Mwandesele
“Siku nyingi tunausubiri huu mradi lakini bado haukamiliki hili ni changamoto kidogo na sisi kwenye vijiji vyetu hatuna kabisa umeme kwa hiyo tunaomba serikali itupe nguvu ili mradi huu uweze kukamilika”alisema Alto Mwakila
Laulent Kiunga ni mwenyekiti wa kijiji cha Kilondo amesema mradi huo unaosimamiwa na wakala wa nishati vijijini (REA) umekwama kutokana na sababu mbali mbali na vifaa vikiwa vimefika huku afisa tarafa ya Mwambao Linus Malamba, akibainisha kuwa mradi huo ni mkubwa kwenye wilaya ya Ludewa utakaoleta faida kwa wananchi wa kata za Kilondo,Lumbila,Ikombe,Matema na kisha kuingizwa kwenye Glidi ya taifa.
Naye Felix Mwakila diwani wa kata ya Kilondo amesema baadhi ya shughuli zimeshafanyika ikiwemo usogezwaji wa vifaa,ununuzi wa mashine,ujenzi wa banio ambao umeishia njiani pamoja na nyumba ya motor lakini fedha za kukamilisha mradi zimekwama.
” wananchi wanahitaji kunufaika kutokana na mradi huu uliopo na malengo ya wananchi ni kuona umeme unawaka kama unavyojua umeme ni maendeleo,tuiombe serikali inusuru wananchi kwa kuwa wanafika wakati wanakata tama na mradi”alisema Felix Mwakila
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga amesema kwa kuwa juhudi za ujenzi wa miundombinu zilishaanza ataendelea kuishauri serikali kukamilisha mradi huo huku hatua za awali zikiwa zimechukuliwa kwa kuwasiliana na REA ili kufanikisha mradi.
“Niliwaomba watu wa REA na walikuja hapa na kuchukua changamoto zote na ni imani yangu kwamba kwenye bajeti hii sasa wataingiza mradi huu kama kipaumbele ili wananchi wa Kilondo nao waweze kupata umeme wa uhakika”alisema Kamonga
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na viongozi wa serikali ya kata,milioni 196 fedha iliyotolewa na serikali imekwisha tumika katika shughuli za mradi huo huku mkandarasi akiwa ameomba milioni 300 kwa ajili kukamilisha mradi utakaozalisha zaidi ya Megawati 25.