…………………………………………………………………………………..
Madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo wanawake pamoja na wauguzi wanawake wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika kuadhimisha siku ya wanawake Duniani tarehe 8, Machi 2021 watafanya upimaji wa magonjwa ya Moyo bila malipo kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam na mikoa jirani. Upimaji huo utaenda sambamba na utoaji wa elimu ya lishe bora kwa afya bora ya Moyo.
Upimaji utafanyika kwa muda wa siku mbili tarehe 04-05/03/2021 kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi jioni katika viwanja vya Mbagala Zakheem vilivyopo wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam kwa kufanya upimaji kwa watu wote. Wananchi watapimwa afya zao za moyo. Kwa wale watakaokutwa na matatizo ya moyo watafanyiwa uchunguzi zaidi na kupatiwa matibabu au kushauriwa rufaa ya kuja kwenye hospitali yetu kwa ajili ya matibabu zaidi ya kibingwa.
Wafanyakazi wanawake wa Taasisi hii tutaendelea kuhakikisha tunatoa huduma bora zaidi za magonjwa ya moyo kwa wananchi. Mpango wetu ni kutoa elimu kwa jamii ambayo itawasaidia wananchi kuwa na ufahamu wa kutosha kuhusiana na magonjwa ya moyo ambayo ni moja ya magonjwa yasiyoambukiza na mtu anaweza kuyaepuka kwa kufuata ushauri wa kitaalamu.
Tunawaomba wananchi mjitokeze kwa wingi kupima afya zenu za moyo hii itakusaidia kujua kama una tatizo mapema na kuanza tiba. Kwani asilimia kubwa ya wagonjwa tunaowapokea katika Taasisi yetu hufika kwa kuchelewa huku tayari mioyo yao ikiwa imeshapata madhara makubwa na kuletea changamoto katika tiba kwa ujumla.