Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akipokea nakala ya hati za utambulisho kutoka kwa Balozi mteule wa Namibia, Mhe. Lebbius Tangeni Tobias leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Balozi mteule wa Ireland mhe. Mary O’Neil akimkabidhi nakala ya hati za utambulisho Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akipokea hati za utambulisho kutoka Konseli Mkuu wa China Zanzibar Mhe. Zhang Zhisheng
***************************************
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amekutana na kupokea nakala za hati za utambulisho za mabalozi wateule hapa nchini pamoja na hati ya utambulisho ya Konseli Mkuu wa China Zanzibar.
Mabalozi waliowasilisha nakala za hati za utambulisho kwa Prof. Kaabudi katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam ni Balozi mteule wa Namibia, Mhe. Lebbius Tangeni Tobias na Balozi mteule wa Ireland mhe. Mary O’Neil, pamoja na Konseli Mkuu wa China Zanzibar Mhe. Zhang Zhisheng.
Awali akiongea mara baada ya kupokea nakala ya hati ya utambulisho wa Balozi mteule wa Namibia, Prof. Kabudi amesema kuwa Tanzania na Namibia zimekubaliana kuendeleza kuimarisha sekta ya biashara na uwekezaji, mifugo na uvuvi katika bahari kuu pamoja madini kwa maslahi ya mataifa yote mawili.
“Tanzania na Namibia tuna historia inayofanana iliyoanza tangu vita vya ukombozi wa uhuru wa Namibia….wote tulikuwa makoloni ya Wajerumani, hivyo tumekubaliana kuimarisha sekta za biashara na uwekezaji, na katika maeneo ya mazao ya mifugo, uvuvi, kilimo, na madini, ambapo katika maeneo hayo Tanzania tunayo mengi ya kujifunza kutoka Namibia hasa katika sekta ya mifugo na uvuvi katika bahari kuu,hivyo tukiimarisha maeneo hayo uchumi wan chi zetu mbili utazidi kukua na kuimarika” Amesema Prof. Kabudi
Kwa upande wake Balozi Mteule wa Namibia hapa nchini, Mhe. Lebbius Tangeni Tobias ameahidi kuendeleza ushirikiano wa kidiplomasia uliopo kati ya Tanzania na Namibia.
“Mimi kama mwakilishi wa Serikali ya Namibia nitajitahidi wakati wa utumishi wangu hapa Tanzania kuhakikisha kuwa uhusiano wetu sisi Namibia na Tanzania unazidi kuimarika kwa maslahi mapana ya wananchi wetu wote,” Amesema Mhe. Tobias
Kadhalika, Prof. Kabudi amepokea nakala ya hati za utambulisho wa Balozi mteule wa Ireland hapa nchini, Mhe. Mary O’Neil ambapo mara baada ya kukabidhi hati za utambulisho Balozi Mteule ameahidi kuendeleza uhusiano mzuri uliopo baina ya Tanzania na Ireland.
“Ni furaha kwangu kuwepo hapa leo na kukabidhi nakala ya hati ya utambulisho wangu hapa nchini Tanzania, napenda kuahidi kwa kipindi nitakachokuwa hapa nitahakikisha kuwa uhusiano wetu wa kidiplomasia unakuwa na kuimarika kwa maslahi ya mataifa yetu,” Amesema Balozi O’Neil
Kwa upande wake Prof. Kabudi amesema kuwa mahusiano ya kibalozi kati ya Tanzania na Ireland yalianza tangu mwaka 1979 ambapo Ireland ilianzisha utaratibu wa kutoa ufadhili wa masomo katika vyuo vikuu vya Ireland kwa watanzania katika taaluma mbalimbali.
“Mbali na kutoe ufadhili wa elimu kwa Watanzania, tumeongelea masuala ya kuimarisha ufadhili wa masomo, biashara na uwekezaji hasa kwa kutumia teknolojia ya habari pamoja na kuimarisha uvuvi wa bahari kuu na katika kipindi chake cha uwakilishi hapa nchini tutaangalia maeneo mapya ya ushirikiano ili tuweze kuendele kuimarisha ushirikiano baina yetu na Ireland,” Amesema Prof. Kabudi.
Katika tukio jingine, Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) amekutana na kupokea hati ya utambulisho wa Konseli Mkuu wa China Zanzibar Mhe. Zhang Zhisheng.
Prof. Kabudi amesema kuwa China imekuwa ikiisaidia sana Zanzibar tangu mapinduzi ya mwaka 1964, katika maeneo mbalimbali kama vile ujenzi wa barabara, ujenzi wa shule, ukarabati wa uwanja wa ndege, hospitali ya Mnazi mmoja pamoja na Abdallah Mzee………na “tumekubaliana kuwa tutaendelea kuimarisha mahusiano kati ya China na Tanzania – Zanzibar ikiwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” Amesema Prof. Kabudi
Nae Konseli Mkuu wa China Zanzibar amesema kuwa China kama taifa lililoendelea wataendelea kushirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha mahusiano ya China na Tanzania yanaimarika kijamii, kisiasa na kiuchumi.
“China inaunga mkono umoja, amani na mshikamano wa Tanzania, sisi tumekuwa marafiki wa muda mrefu na tutaendelea kusaidiana ili kuhakikisha kuwa mahusiano kati ya China na Tanzania yanazidi kuimarika hasa katika kipindi hiki cha uongozi wa Rais Magufuli na Rais Mwinyi,” Amesema Mhe. Zhisheng