Dkt. Paul F. Kihwelo, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto akizungumza wakati wa kufungua mafunzo elekezi kwa Mahakimu Wakazi wapya 70 waliohudhuria mafunzo hayo Chuoni Lushoto
Baadhi ya washiriki wa Mafunzo Elekezi wakiwa wanasikiliza moja ya mada katika mafunzo hayo yaliyoandaliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania na yanaendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
January Msofe, Jaji Mstaafu wa Mahakama ya Rufani akitoa mada kwa washiriki wa mafunzo elekezi ambayo yameandaliwa na Mahakama Kuu ya Tanzania na yanaendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
***************************************
Mhe. Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dkt Eliezer Mbuki Feleshi amewataka mahakamu wapya 70 kuhakikisha wanatoa haki kwa wote na kwa wakati. Pia amewataka mahakimu hao kwenda kuwa mwarobaini wa kutoa suluhisho kwenye maeneo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wananchi katika mahakama za mwanzo, hasa mashauri ya mirathi.
Mhe. Jaji Dkt Feleshi aliyasema hayo kwenye hotuba yake iliyosomwa na Mhe. Dkt. Paul Faustin Kihwelo, Jaji wa Mahakama Kuu na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wakati wa kufungua semina hii elekezi kwa Mahakimu Wakazi wapya 70.
Mhe. Jaji Kiongozi aliongeza kuwa, mafunzo watakayopewa ni muhimu na yamelenga kuwapa mbinu na nyenzo sahihi za kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali wakati wa kuamua mashauri yatakayoletwa mbele yao ili waweze kuyashughulikia kwa mujibu wa mipaka ya kisheria.
Aidha Mhe. Dkt. Feleshi aliwasisitizia juu ya umuhimu wa kujinoa katika matumizi ya TEHAMA ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia katika utoaji wa haki kwa wakati.
“kwa kuwa tunaishi katika mapinduzi ya nne ya viwanda mnasisitizwa kujinoa zaidi kwenye matumizi ya TEHAMA na mifumo ya kielektroniki tuliyonayo mahakamani ili tuweze kuendana na kasi ya mabadiliko ya kidunia hivi sasa “
Hata hivyo hakusita kuwakumbusha juu ya kuzingatia matumizi sahihi ya lugha katika utendaji wao wa kazi ikiwa ni sanjari na uwepo wa uhitaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili ambayo itatumiwa Mahakamani na kuwahimiza kujisomea stadi za lugha ili kuongeza misamiati ya kisheria kwani itatoa wigo mpana katika kukuza lugha ya Kiswahili cha kisheria.
Kwa upande wake, Mhe. Wilbert Chuma, Msajli Mkuu wa Mahakama ya Tanzania aliwakumbusha mahakimu hao wapya kufanya kazi kwa uadilifu na weledi ili kujiepusha na mazingira ya rushwa ili kulinda heshima ya Mahakama.
Mahakimu hao waliaapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma Februari 26, 2021 katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam.