Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Moses Chitama, akifungua mafunzo yanayohusu masuala ya ununuzi na usimamizi wa mikataba kwa wajumbe wa Menejimenti ya TSC, Machi 1, 2021 mjini Morogoro.
Mwezeshaji wa mafunzo yanayohusu masuala ya ununuzi na usimamizi wa mikataba, Joyce Msangi, akitoa mafunzo husika kwa wajumbe wa Menejimenti ya Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Machi 1, 2021 mjini Morogoro.
Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi, Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Lameck Mbeya, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo yanayohusu masuala ya ununuzi na usimamizi wa mikataba kwa wajumbe wa Menejimenti ya TSC, Machi 1, 2021, mjini Morogoro.
Mkurugenzi Msaidizi wa Utawala, Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Apsa Othman, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo yanayohusu masuala ya ununuzi na usimamizi wa mikataba kwa wajumbe wa Menejimenti ya TSC, Machi 1, 2021, mjini Morogoro.
Washiriki wa mafunzo yanayohusu masuala ya ununuzi na usimamizi wa mikataba kutoka Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), wakifuatilia mada zilizokuwa zikiwasilishwa katika siku ya kwanza ya mafunzo hayo, Machi 1, 2021, mjini Morogoro.
……………………………………………………………………………….
Na Veronica Simba – TSC
Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Moses Chitama amewataka watumishi wa Tume hiyo kuhakikisha kuwa ununuzi wote wa umma unafanyika kwa kuzingatia misingi ya uadilifu.
Ameyasema hayo leo Machi 1, 2021 mkoani Morogoro wakati akifungua mafunzo yanayohusu masuala ya ununuzi na usimamizi wa mikataba kwa Wajumbe wa Menejimenti ya TSC.
Akifafanua, Chitama ameeleza kuwa ununuzi wa umma ukifanyika kwa uadilifu, utawezesha kufikia malengo ya Taifa ya kupata thamani halisi ya fedha ya Serikali inayotumika katika ununuzi.
“Ununuzi wa Umma una mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa letu, hasa ukizingatia kuwa takribani asilimia 70 hadi 80 ya bajeti ya serikali, inakwenda katika ununuzi wa vifaa, kazi za ujenzi na huduma mbalimbali. Hivyo ni muhimu ununuzi ufanyike kwa ufanisi,” amesisitiza.
Kaimu Katibu amewakumbusha washiriki wa mafunzo husika kuwa, Serikali imejikita katika kudhibiti matumizi ya fedha za umma, hivyo inafanya kila jitihada katika kuhakikisha kuwa fedha hizo zinatumika kwa ufanisi.
Aidha, amesema kuwa, pamoja na kwamba wapo wataalamu wa ununuzi wanaowajibika moja kwa moja kufanya kazi hiyo, hata hivyo uongozi wa TSC umeona ni vyema kutoa mafunzo husika kwa viongozi na wataalamu wa kada nyingine mbalimbali, hususani wale wanaotoa maamuzi katika hatua mbalimbali za ununuzi.
Amefafanua kuwa mafunzo hayo yatawajengea uwezo viongozi na wataalamu husika, waweze kushirikiana kwa ufanisi katika utekelezaji pamoja na kuepuka hoja mbalimbali za ukaguzi ambazo hujitokeza pale taratibu za ununuzi zisipofuatwa kikamilifu.
Mafunzo hayo ya siku tano, yanatolewa kwa mujibu wa Sheria ya Ununuzi wa Umma namba 7 ya mwaka 2011, pamoja na Kanuni zake, tangazo la serikali namba 446 la mwaka 2013, ikisomwa pamoja na marekebisho yaliyofanyika mwaka 2016.
Wanaoshiriki mafunzo hayo ni Menejimenti, Wajumbe wa Bodi ya Zabuni pamoja na Maafisa Ununuzi ambao ndiyo huhusika katika kutoa maamuzi wakati wa shughuli za ununuzi na usimamizi wa mikataba katika Taasisi husika (TSC).