………………………………………………………………………….
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani kimetoa cheti cha pongezi kwa Rais Dk John Magufuli kwa kufanikisha ushindi wa chama hicho kushika dola,kwa kipindi kingine cha miaka mitano.
Aidha cheti kingine kilitolewa kwa Rais Mstaafu wa awamu ya nne Dk Jakaya Kikwete ambacho alikabidhiwa kabla ya mkutano huo.
Zawadi hiyo kwa Rais na aliyekuwa katibu wa CCM Taifa Dk Bashiru Ally Kakurwa ambaye ilikabidhiwa na mwenyekiti wa Ccm mkoa Ramadhan Maneno kwa mlezi wa chama hicho Mkoa wa Pwani Gaudencia Kabaka wakati kikao maalum cha Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa.
Watu wengine waliopewa vyeti vya shukrani ni pamoja na wabunge wa mkoa huo na wale waliogombea nafasi hiyo, mkuu wa mkoa, wakuu wa wilaya, wakurugenzi wa halmashauri za Mkoa huo, wenueviti wa CCM wilaya za Mkoa huo na wadau waliokiwezesha chama kushinda nafasi za urais, ubunge na udiwani.
Akizungumza kwenye kikao hicho mlezi wa Ccm Mkoa wa Pwani ,Gaudencia Kabaka alisema kuwa licha ya changamoto iliyojitokeza ya utaratibu wa kadi za kieletroniki kutokamilika wawatambue wanachama kwa kadi za zamani.
“Ukosefu wa kadi za kieletroniki isisababishe mambo mengine yasiendelee kwani zoezi hilo litakamilika hivyo msiwe na wasiwasi juu ya kadi hizo za kisasa,” alisema Kabaka.
“Tuwe wavumilivu chama kiko vizuri na tunaelekea vyema na tunamshukuru Rais kwa kuhakikisha nchi inakwenda na kuwaletea maendeleo wananchi,” alisema Kabaka.
Naye mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani Ramadhan Maneno alieleza,kumekuwa na changamoto mara uchaguzi unapokwisha kutokana na makundi ya wagombea na kusababisha mitafaruku ya hapa na pale.
Naye Katibu wa Ccm mkoa wa Pwani Elia Mpanda akizungumzia juu ya kadi hizo za kieletroniki alisema taratibu zinaenda vizuri hivyo wanaccm na viongozi wasiwe na hofu.
Mpanda alisema ,teknolojia ina changamoto zake lakini haitasababisha kurudi nyuma katika mchakato wa kwenda kisasa.