Apolinary Macheta Makam Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Suumbawanga akisikiliza kwa makini mada mbalimbali zinazoendelea katika kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Rukwa.
mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa nasaha zake wakati wa kufunga kikao cha bodi ya Barabara Mkoani Rukwa.
Mbunge wa Kwela Mh. Deus Sangu pamoja na Mbunge wa Nkasi Kaskazini Mh. Aida Khenan wakiendelea kufuatilia mada mbalimbali zinazoendelea katika kikao cha bodi ya Barabara Mkoani Rukwa kilichofanyika tarehe 22.2.2020.
Makam Mwenyekiti wa Bodi ya Barabara mkoa wa Rukwa ambaye pia ni mbunge wa Kalambo Mh. Joasephat Kandege (wa kwanza kulia) akiwa meza moja na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo.
******************************************
Wajumbe wa Bodi ya Barabara Mkoani Rukwa wamesikitishwa na kitendo cha Wakala wa Barabara za Mijini na Vijini (TARURA) Pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROAD) kushindwa kuonyesha mpango wa kufungua barabara zinazoelekea ziwa Rukwa hasa katika maeneo ambayo utafiti unaonesha kuwa kuna gesi ya Helium inayoweza kuchimbwa.
Akiibua hoja hiyo katika kikao cha Bodi hiyo Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri Ya Wilaya ya Sumbawanga Mh. Apolinary Macheta alisema kuwa hapo awali katika bonde la Ziwa Rukwa kulikuwa na njia za kuelekea katika ziwa Rukwa lakini hivi sasa hakuna na hivyo kuiomba serikali kuona umuhimu wa kutenga bajeti kwaajili ya kuweka miundombinu Rafiki kwaajili ya kufika katika mradi huo wa helium.
“Lakini Mheshimiwa Mwenyekiti ukiangalia kuanzia (Kijiji cha) Muze, Uzia – Kijiji kimoja kutoka Muze, kama nilivyosema zamani kulikuwa na njia magari yanaweza yakaingia huko ziwani, (lakini sasa) hakuna hata njia moja, hivyo nadhani jambo hili tulione kwa kina sana,” Alisema.
Akichangia hoja hiyo mbunge wa Nkasi Kaskazini Mh. Aida Khenan alisema kuwa haiwezekani kuifikia gesi hiyo endapo miundombinu sio rafiki na hivyo kutoa kutoa ushauri kwa TARURA juu ya kuweka vipaumbele vya ujenzi wa barabara ambazo zitachochea ukuaji wa uchumi wa Mkoa wa Rukwa.
“Tunazungumzia (mkoa) Songwe, wanaichukua hiyo fursa kwa maana gani, kama wameona sisi hatusemi lazima wafanye hivyo na mwisho wa siku wataanza kunufaika Songwe badala ya Rukwa, nilikuwa nashauri tena Pamoja na kwamba kuna brabara ambazo ni korofi sana, lakini lazima tuangalie kwanini tupeleke fedha pale, tunapeleka pale kwasababu barabara hii ikikamilika, vichocheo vya uchumi vinavyopita kwenye hii barabara vinaweza kutengeneza barabara nyingine,” Alisema.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Kwela Mh. Deus Sangu alishauri bajeti ya TARURA kuwa na fungu la kuwezesha kujenga barabara zinazoelekea katika ziwa Rukwa kutokana na umuhimu na uharaka wake na kuiwasilisha Wizarani na hivyo ngazi ya mkoa kujivua lawama na kulibakisha mikononi mwa wizara husika na wenye maamuzi.
“Niwaombe TARURA mwaka huu wa fedha uwe ni mwaka wa mwisho kuwa na ‘Template’ ya aina hii (ya bajeti) tubadilishe mkafanye ‘survey’ mpya ya barabara, mje na mahitaji yaliyo halisi, tupeleke mahitaji yaliyo halisi siyo kukariri mambo ya miaka ya 2007 kwamaba milioni 600 ndio ‘Ceiling’ mwengine ana Shilingi bilioni 1.5 hatutafika,” Alieleza.
Katika kukazia hilo Mwenyekiti wa Bodi hiyo ambaye pia ni Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo alisema kuwa Mkoa wa Rukwa umejaaliwa kuwa na rasilimali kubwa ya gesi ya Helium na endapo miundombinu ya kufikia gesi hiyo sio Rafiki, wawekezaji watashindwa kufika katika maeneo hayo.
“Ni lazima barabara hizi zipitike na kwa namna ile ni lazima zipate fedha za kutosha kutoka wizara inayohusika, vinginevyo tutakuwa tunazungumza tu ‘Helium gas’ umuhimu wake lakini hatuwezi kuichima ile gesi kwasababu ya barabara, kwahiyo ni lazima TANROAD na TARURA waongeze bajeti ya barabara zao, hususan kwenye bonde la ziwa Rukwa ili hiyo ‘Helium gas’ tuweze kuizungumzia vizuri katika kuichimba na kuitangaza, hatuwezi kuitangaza kama wawekezaji hawawezi kufika kwasababu ya kutokuwepo kwa barabara,” Alisisitiza.
Kwa mwaka wa fedha 2021/2022 TARURA wameomba kupitishiwa bajeti ya Shilingi 38,544,061,553.75 kwaajili ya matengenezo ya barabara ikijumuisha fedha za matengenezo Shilingi, 4,119,774,160.83 na Shilingi 34,424,287,392.92 kwaajili ya miradi ya maendeleo kwa barabara zenye urefu wa km 450.37 kwa matengenezo ya barabara na vivuko mchanganyiko 51.