****************************************
NA DENIS MLOWE,IRINGA
CHAMA cha Mapinduzi wilaya ya Iringa Mjini kimempa tuzo ya heshima Mjumbe wa Halmashauri kuu CCM Taifa Salimu Abri Asas ikiwa ni mchango wake katika kusaidia jamii na kukisaidia kwa kiasi kikubwa chama hicho Nyanda za juu kusini kuibuka na ushindi wa kishindo katika uchaguzi mkuu wa 2020.
Akizungumza kwenye kikao cha halmashauri kuu ya wilaya hiyo, Mwenyekiti wa CCM wilaya, Said Rubeya alisema kuwa mchango mkubwa aliotoa Salim Abri kwa jamii ya watu wa Iringa na baadhi ya mikoa ya jirani na ndani ya chama hakuna mfanowe hali ambayo wamelazimika kumpa tuzo hiyo heshima kuthamini mchango wake.
Rubeya alisema kuwa Salim amekuwa na mchango kwa jamii na mtu mmoja mmoja bila kuangali itikadi ya chama anachotoka hali ambayo imemfanya kuwa mtu wa kipekee sana katika jamii inayomzunguka.
Alisema kuwa katika kuhakikisha maendeleo yanapatikana Salim Abri amekuwa akijitokeza kwenye kila jambo ambalo linahitaji mchango wake na kila sekta amegusa jamii ikiwemo sekta ya afya, sekta ya elimu na bado amekuwa mfano bora kwa kampuni anazozioongoza kudhamini watu mbalimbali na sekta ya michezo.
Aliongeza kuwa ushindi mkubwa uliopatikana kwa mikoa ya nyanda za juu kusini umechangiwa ka kiasi kikubwa na ushirikiano wake na chama kwa kutoa misaada mbalimbali iliyofanikisha kampeni licha ya kufanya kampeni kwa mikoa yote ya nyanda za juu Kusini.
Aidha Rubeya aliwataka viongozi wa chama na wanachama kuacha kubweteka na ushindi uliopata na kuhakikisha wanawatumikia wananchi waliowachagua katika kuwaletea maendeleo.
Kwa upande wake Salim Abri licha ya kushukuru tuzo hiyo alisema kwamba ataendelea kuwasaidia wananchi wa Iringa pamoja na kukitumikia Chama Cha Mapinduzi CCM kwa moyo wake wote na hataacha kusaidia maendeleo ya mkoa wa Iringa kwa kuwa ni mzaliwa wa hapo.
Asas alisema kuwa kamwe hatayumbishwa,wala kukatishwa tamaa na mtu yeyote wakiwemo watu wanaomkashifu katika mitandao ya kijamii bila sababu ya msingi na kuwa na ugonjwa wa Salimphobia kwani kila siku watu wakiamka wao na yeye tu.
“sitarudishwa nyuma wala kuyumbishwa na watu wenye huo ugonjwa wa Salimphobia kwani nitaendelea kukitumikia Chama Cha Mapinduzi CCM na sitahofia maneno ya uzushi kwani sitishiki na siogopi mtu mwenye nia mbaya na maneno machafu kwangu “ alisema