***************************************
Nteghenjwa Hosseah, Dar es Salaam
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI Eng. Joseph Nyamhanga amemuelekeza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam kuhakikisha kuwa machinjio ya vingunguti inaanza kutoa huduma mapema mwezi March,2021.
Eng. Nyamhanga ameyasema hayo alipotembelea kukagua maendeleo ya ujenzi wa Machinjio hiyo ya Kisasa na kubaini ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 98.
“ Kwa kuwa ujenzi wa machinjio hii umeshakamilika kwa kiwango cha kuanza kutoa huduma sasa inatakiwa kazi zianze hata kwa kuchinja ng’ombe,mbuzi na kondoo wachache mpaka hapo mtakapokamilisha ujenzi kwa asilimia 100” alisema.
Pia alieleza kuwa Machinjio za Kisasa zinajengwa katika Halmashauri 7 Nchini lengo ikiwa kuzijengea uwezo Halmashauri ziweze kujitegemea kimapato.
Alitaja maeneo ambayo Machinjio hizo zinajengwa kuwa ni Manispaa ya Lindi, Sumbawanga,Shinyanga,Songea,Mpanda,Iringa na Halmashauri ya Mji wa Geita.
‘Machinjio hii ikianza kutoa huduma itakua inakusanya Bil 2 mpaka Bil 5 kwa mwaka sasa mapato hayo yatawezesha Jiji la Ilala kupunguza utegemezi kwa Serikali na kutekeleza miradi ya maendeleo na kutoa huduma bora kwa Wananchi’ alisema Nyamhanga.
Pia Eng. Nyamhanga aliutaka Uongozi wa Jiji hilo kuanzisha Kampuni(Special purpose vehicle) kwa ajili ya kuendesha Machinjio ya Vingunguti.
Naye Mkurugenzi wa Jiji la Dar es salaam Jumanne Shauri amsema mpaka sasa wameshaajiri wafanyakazi 150 na wameanza mafunzo kwa vitendo kwa muda wa miezi miwili sasa ili waweze kuelewa vizuri kazi hiyo kwa kuwa walitoka kwenye machinjio ya kawaida na sasa wamekuja kwenye machinjio ya kisasa.
‘Tumeajiri wafanyakazi 150 na tukaongeza wengine 150 hivyo tutakua tumetoa ajira za moja kwa moja 300 na zile zisizo za moja kwa moja zitaka 3000 kwa maana ya wale wanaoleta mifugo, wafanyabiashara wanaokuchukua nyama kupeleka buchani pamoja na wale watakaosafirisha nyama hizo’ alisema.
Pia Mkurugenzi Shauri alitaja gharama za mradi kuwa ni shilingi Bil 12.4 kwa kazi za ndani na za nje pamoja na kufunga mitambo yote.
Aliweka wazi kuwa machinjio hiyo itafanya kazi kisasa na watatengeneza sausage pamoja na nyama ya kusaga.
Naye Meneja wa Ujenzi wa Machinjio ya Vingunguti Eng. Mburuga Matamwe amesema mradi umekamilika kwa Hatua asilimia 98 kwa kazi za ndani na za Nje.
Alieleza uwezo wa machinjio hiyo kuwa ina uwezo wa kuchinja ngombe 1,500 kwa siku huku mbuzi na kondooo ni 3000 kwa siku.