……………………………………………………………………………….
Mwandishi wetu, Kigoma
Kaya zaidi ya 100 za Wakulima na wafugaji wengi wakitoka nchi jirani, wamevamia eneo la hifadhi ya ardhi oevu Moyowosi- Malagarasi ,wilayani Kasulu mkoa wa Kigoma na kufungua mashamba makubwa ya mpunga na mahindi huku mifugo ikiharibu hifadhi hiyo ya kipekee duniani.
Wakizungumza na waandishi wa habari, baadhi ya viongozi wa serikali na wadau wa Uhifadhi na Utalii, walisema jitihada za haraka zinahitajika kuokoa eneo hilo ambalo ni muhimu kwa uchumi wa Taifa .
Mkuu wa wilaya ya Kasulu,Kanali Simon Anange alisema operesheni ya kuwaondoa wavamizi hao inatarajiwa kufanyika mwezi ujao, lakini suluhu ya kudumu ni kulipandisha hadhi eneo hilo ili liweze kulindwa na maafisa wa TAWA muda wote kwani sasa lipo chini ya halmashauri ya Kasulu ambao walinzi wa kutosha.
“kuna watu wamevamia kulima na kuanza kufuga katika eneo hili muhimu kwa uchumi wa taifa,tumewataka kuondoka kwa hiari bado kuna ambao wamekaidi hivyo taratibu zinafanywa kuwaondoa na raia halali watahamishiwa eneo la Kagerankanda ambalo limetolewa na serikali”alisema
Meneja wa kitalu cha Uwindaji cha Makare forest eneo la wazi la uvinza kilichopo katika eneo hilo, Dago Ally alisema wavamizi wengi raia ya nchi jirani, wameanzisha mashamba na kuingiza mifugo katika eneo hilo.
Ally alisema wavamizi hao wana makundi makubwa ya mifugo zaidi ya 5000 wamefungua mashamba makubwa ya mahindi na mpunga ndani ya eneo la hifadhi jambo ambalo ni hatari.
Mkuu wa idara ya kuzuia ujangili katika kitalu hicho, alisema wavamizi hao licha ya kulima na kufunga pia wamekuwa wakijihusisha na matukio ya ujangili na tayari baadhi wamekamatwa na nyamapori na silaha mbali mbali.
“tumefanya operesheni mara kadhaa kukamata mifugo na silaha kutoka kwa wavamizi ambao wengi ni watusi lakini tunakwamishwa na baadhi ya wanasiasa ambao ndio wamekuwa wakiwapokea”alisema
Meneja wa Pori la Akiba la Moyowosi, ,Bigiramungu Kagoma alisema, eneo hilo ambalo linapakana na pori la akiba la Moyowosi ni muhimu kwa ajili ya uhifadhi kwani kuna wanyama kama Zohe, Statunga na ndege aina ya Korongo nyangumu ambao hawapatikani sehemu nyingi duniani.
“eneo hili likiendelea kuhifadhiwa sio tu litalinda kawa wanyama na ndege lakini pia ikolojia yote ya Moyowosi na Malagarasi itakuwa salama na ziwa Tanganyika litalindwa”alisema
Mmoja wa wavamizi, Juma Malilo ambaye ni mfugaji alisema wamehamia katika eneo hilo kufuata malisho na ardhi na hawajuwi kama ni hifadhi kwani wamekaribishwa na viongozi wa vijiji.