Diwani wa kata ya Namasakata katika Halmashauri ya wilaya Tunduru Rashid Usanje kushoto akimtwisha ndoo ya maji mkazi wa kijiji cha Namasakata Hadija Namtunga baada ya kutembelea mradi wa maji uliotekelezwa na wakala wa maji safi na uhifadhi wa mazingira(Ruwasa)wilayani humo ambao umesaidia kurudisha huduma ya maji safi na salama iliyokosekana kwa miaka zaidi ya 25 na wananchi wa kijiji hicho walilazimika kutumia maji ya visima vya asili kwa matumizi yao ya kila siku.
Picha na Muhidin Amri
*****************************************
Na Muhidin Amri,
Tunduru
WIZARA ya maji kupitia wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini Ruwasa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,imetekeleza mradi mkubwa wa maji katika kijiji cha Namasakata utakao wanufaisha zaidi ya wakazi 5,500 wa kijiji hicho.
Meneja wa Ruwasa wilayani hapa Primy Damas alisema, mradi huo umejengwa kwa kutumia force akaunti na awali gharama ilikuwa shilingi 17,335,720 lakini baada ya mapitio gharama iliongeza hadi kufikia shilingi 19,065,720 na umekamilika kwa asilimia 98.
Katika mradi huo kazi zilizopangwa kufanyika na zilizofanyika ni ukarabati wa tenki la chini la lita za ujazo 158,000,ujenzi wa nyumba ya mitambo,ununuzi wa mabomba zenye ukubwa tofauti za umbali wa mita 5,800 na viungio vya mabomba.
Damas alisema, mbali na hizo kazi nyingine zilizofanyika ni ununuzi na ufungaji wa nishati na mfumo wa umeme wa jenereta,ununuzi na ufungaji wa pampu ya kisima,uchimbaji mitaro,uchimbaji mabomba na ufukiaji mitaro umbali wa mita 5,800 na ujenzi wa vituo 11 vya kuchote maji vyenye koki mbili kila kimoja.
Kwa upande wake fundi sanifu wa mradi huo Emmanuel Mfyoyi alisema, ili kuhakikisha mradi unafanya kazi na wananchi wanapata maji muda wote wamefunga jenereta la kilowati 15 lenye uwezo wa kupandisha maji kwa masaa 24 kwenda kwenye tenki kwa kutumia pampu iliyopo ambayo inatumia mafuta kidogo.
Amewahakikishia wananchi wa kijiji hicho kuwa, sasa watapa maji safi na salama wakati wote na kuwataka kutunza mradi huo ambao umefanikisha kumaliza kero ya maji kwa wananchi hao iliyokuwepo kwa muda mrefu.
Diwani wa kata ya Namasaka Rashid Usanje alisema, sasa wanajivunia kuona kijiji hicho kina maji ya uhakika ambapo wananchi hawana tena kero ya kwenda umbali mrefu kufuata maji kwenye visima vya asili na mito inayozunguka kijiji hicho.
Alisema, miaka ya nyuma kijiji hicho kiliwahi kupata mradi wa visima vya maji kupitia mradi wa Chip uliopo chini ya kanisa la Anglikana Doyasisi ya Tunduru Masasi, hata hivyo kutokana na kuongezeka kwa idadi kubwa ya watu na kutofanyiwa ukarabati wa mara kwa mara visima hivyo vilikufa tangu miaka ya tisini.
Alisema, tangu wakati huo wananchi waliendelea kuteseka kwa kukosa maji ambapo walilazimika kutumia masaa 2 hadi 3 kwenda kwenye vyanzo vya asili kwa ajili kutafuta maji.
Mwenyekiti wa kijiji hicho Rashid Machele, ameishukuru Serikali kupitia Ruwasa kujenga na kukamilisha mradi huo ambao umesaidia sana kumaliza kero ya maji kwa wananchi.
Alisema, mradi huo umeleta faraja kwa wananchi na kupunguza matukio ya watu kuliwa na kujeruhiwa na wanyama wakali kama tembo,simba na chui pindi wanapokwenda na kurudi kutafuta maji kwa matumizi yao ya kila siku.
Adija Namtunga alisema, awali tatizo la maji katika kijiji hicho lilisababisha sana kurudisha nyuma ya maendeleo yao kwani walilazimika kutumia mwingi kwenda kutafuta maji badala ya kutumia katika shughuli nyingine za maendeleo.
Ameipongeza Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kutekeleza kwa vitendo ilani yake ya uchaguzi ya mwaka 2015 ambayo imewasaidia sana wananchi pamoja na kutekeleza kauli mbiu ya kumtua ndoo mama kichwani.