Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisalimiana na Mkuu wa wilaya ya Njombe Ruth Msafiri alipowasili katika mkoa wa Njombe tarehe 25 Februari 2021 kwa ajili ya kikao kazi na watendaji wa sekta ya ardhi pamoja na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo. Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na Mkuu wa mkoa wa Njombe Mhandisi Mwita Rubirya alipowasili katika mkoa wa Njombe kwa ajili ya kikao kazi na watendaji wa sekta ya ardhi pamoja na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa huo tarehe 25 Februari 2021.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi na Wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Njombe (hawapo pichani) wakati wa kikao kazi katika ziara yake ya siku moja katika mkoa huo. Wa pili kulia ni Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Njombe Christopher Mwamasage.
Sehemu ya watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Njombe wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (hayupo pichani) wakati wa kikao kazi na watendaji hao na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Njombe tarehe 25 Februari 2021.
Mkuu wa wilaya ya Ludewa Andrea Tsere akichangia maoni wakati wa kikao kazi kati ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula na watendaji wa sekta ya ardhi katika mkoa wa Njombe tarehe 25 Februari 2021.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na wananchi aliowakabidhi hati za ardhi wakati wa kikao kazi na watendaji wa sekta ya ardhi na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Njombe tarehe 25 Februari 2021, Wa pili kulia ni Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Njombe Christopher Mwamasage na kulia kwa Naibu Waziri ni Msajili wa Hati Msaidizi Benedict Nsaji. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA WIZARA YA ARDHI)
*****************************************
Na Munir Shemweta, NJOMBE
Wakati Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ikifanya jitihada mbalimbali kuhakikisha sekta ya ardhi inapiga hatua katika kupanga, kupima na kumilikisha ardhi, mkoa wa Njombe kupitia halmashauri zake umeonekana kuwa nyuma katika juhudi hizo na kumfanya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kutoridhishwa na utoaji huduma za sekta ya ardhi katika mkoa huo.
Hali hiyo imebainika wakati wa kikao cha kazi baina ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Mabula na watendaji wa sekta ya ardhi pamoja na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Njombe kilichofanyika tarehe 25 Februari 2021 katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe.
Akisoma taarifa ya utekelezaji kazi za ofisi ya ardhi mkoa wa Njombe, Kmaishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Njombe Christopher Mwamasage alisema, tangu kuanzishwa ofisi ya ardhi mkoa mwezi Machi, 2020 ofisi hiyo imetekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo kuandaa michoro 59 ya Mipango Miji. Hata hivyo, halmashauri za Makete na Ludewa katika taarifa yake zimeonesha kutofanya vizuri kwa kushindwa kuidhinisha hata mchoro mmoja.
Aidha, halmashauri za Makete, Ludewa na ile ya Njombe zimeshindwa pia kufanya lolote katika zoezi la urasimishaji makazi huku katika utekelezaji kazi za upimaji na ramani mkoa ukiwa umeidhinisha mashamba 3 pekee na halmashauri ya wilaya ya Njombe ikiidhinisha ramani na kiwanja kimoja na halmashauri Makete ikiwa haina mchoro wala kiwanja ilichoidhisha.
Katika zoezi la utoaji hati na makusanyo ya kodi ya pango la ardhi, Mwamasage alisema jumla ya hati 1,136 zilisainiwa na mkoa ulikusanya shilingi 774,346,269 kati ya Bilioni 5.3 ilizopangiwa kukusanya mwaka wa fedha 2020/2021 huku mkoa ukipeleka wadaiwa sugu wa kodi ya pango la ardhi 22 katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya wanaodaiwa shilingi 294,930,957.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula alionesha kutoridhishwa na huduma za sekta ya ardhi zinazotolewa katika mkoa wa Njombe na Kuzijia juu halmashauri za wilaya za Makete na Ludewa kwa nyuma sana katika kutekeleza majukumu ya sekta ya ardhi.
‘’Hakuna eneo linalohitaji urasimishaji, umilikishaji hata wa mashamba, hata hati za kimila hii inasikitisha sana na kwa staili hii hatuwezi kufika, yaani Makete sifuri hakuna chochote, kwa hali hii mnawasaidiaje wananchi?’’ alisema Dkt Mabula
Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Ardhi, kwa mwenendo uliooneshwa na halmashauri za Makete na Ludewa haina maana ya kuwa na ofisi za ardhi za mkoa na kusisitiza kuwa baadhi ya wakurugenzi wa halmashauri wanaona hali hiyo ni sawa wakati wao ni mamlaka za upangaji katika maeneo yao.
Aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi kubadilika na kufanya kazi kwa weledi na kujitahidi kufanya vizuri katika utendaji kazi ambapo aliwaeleza kuwa kila Mkuu wa Idara ya Ardhi ama Afisa ardhi Mteule atapimwa kutokana na utendaji wake ikiwemo kiasi cha fedha alizokusanya katika kodi ya pango la ardhi.