**************************************
NA EMMANUEL MBATILO, MTWARA
Jumla ya wanafunzi thelathini na tisa (39) wenye ufaulu wa juu daraja la kwanza na la pili katika fani za Uchumi na Fedha wamekwishanufaika na mfuko wa ufadhili wa Gilman Rutihinda katika masomo yao ya shahada za uzamili.
Kati yao wanufaika saba ni wanawake, na wanufaika thelathini na mbili (32) ni wanaume.
Ameyasema hayo jana Meneja wa Mafunzo BoT Bi.Suzana Mgasa akiwasilisha Mada katika Semina kwa waandishi wa habari za fedha,Uchumi na Biashara mkoani Mtwara.
Akizungumza katika semina hiyo Bi.Suzana amesema katika wanafunzi hao 39 wanufaika thelathini na tano (35) wameshakamilisha masomo hayo kwa ufaulu wa juu na wanalitumikia taifa katika njanja mbalimbali na kati yao, wanufaika Nane (8) ni waajiriwa wa Benki kuu ya Tanzania wakiwemo wakurugenzi, mameneja na wataalamu ambao ni maafisa katika ngazi mbalimbali.
Aidha amesema kuwa ufadhili hutolewa kila mwaka kwa wanafunzi wawili (2) wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam waliomaliza shahada ya kwanza katika fani ya Uchumi na Fedha na kupata ufaulu wa juu (Best performers).
“Majina ya wanafunzi wenye ufaulu wa juu katika fani hizo huchukuliwa moja kwa moja toka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kwenye vitengo husika”. Amesema