Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mhe. Zephania Chaula (kulia) akimwongoza Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda ( kushoto) kukagua maeneo ambapo nzige wa jangwani wameuawa baada ya kupuliziwa kiuatilifu kwenye mapori ya kijiji cha Losokonoi wilaya ya Simanjiro.
Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda (kulia) akisikiliza maelezo kuhusu zoezi la kudhibiti makundi ya nzige toka kwa mtaalam wa wizara ya Kilimo Bw. Joshua Muro (kushoto) jana wakati alipokagua ufanisi wa kazi hiyo kwenye kijiji cha Losokonoi wilaya ya Simanjiro.
Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda ameridhishwa na kazi ya kuangamizwa makundi ya nzige kwenye wilaya za Simanjiro, Siha na Longido kufuatia ndege maalum kunyunyizia kiuatilifu na kuua nzige hao wa jangwani.
Akiwa kwenye ziara ya kukagua utekelezaji wa zoezi la kuangamiza makundi ya nzige jana (24.02.2021) kwenye wilaya za Simanjiro na Siha Prof. Mkenda alishuhudia makundi ya nzige waliokufa baada ya kupuliziwa kiuatilifu (sumu) kazi iliyofanywa na wataalam wa wizara ya kilimo kwa ushirikiano na wataalam wa wilaya hizo.
“Tunawashukuru watalaam wetu wa kilimo kwa kazi nzuri ya kudhibiti makundi ya nzige licha ya ugumu wa mazingira ya kuingia vichakani na kuangamiza nzige porini .Nimeshuhudia nzige wengi wamekufa” alisema Waziri Mkenda
Akiwa kwenye kijiji cha Landanai kata ya Lokosonoi wilaya ya Simanjiro Prof. Mkenda alijionea makundi ya nzige waliokufa kufuatia zoezi la kuwapulizia dawa kwa njia ya ndege pia mabomba ya kupulizwa kwa mikono iliyofanywa na wataalam wa kilimo.
Akizungumza kuhusu mikakati ya kudumu ya kudhibiti wadudu waharibifu wa mazao ikiwemo nzige na kwelea kwerea, Waziri Mkenda alisema wizara itaanzia Idara ya Kilimo Anga ambapo kwenye bajeti ya mwaka huu itatenga fedha za kununua ndege (drones) kwa ajili ya kunyunyizia viuatilifu pale makundi ya wadudu waharibifu yatakapotokea nchini.
Amewahakishia wakulima na wafugaji nchini kuwa serikali iko makini kuhakikisha nzige na visumbufu vingine vya mazao na malisho ya mifugo vinaangamizwa na kuwa viautilifu kwa ajili ya kazi hiyo vipo nchini.
“Suala la kupambana na nzige wa jangwani ni kama vita lazima tushirikiane wote ikiwemo nchi jirani ya Kenya kuwateketeza hivyo nitawasiliana na wenzetu kujua namna wanavyofanya kazi ya kuangamiza nzige ili wasije kuingia kwenye mipaka yetu” alisisitiza Prof. Mkenda
Kwa upande wake Mtaalam wa kudhibiti visumbufu toka Wizara ya Kilimo Joshua Muro anayeongoza zoezi la kuangamiza nzige Simanjiro alisema zoezi limeanda vema licha ya ugumu wa kupita vichakani kufuatilia kujua makundi ya nzige ambapo kazi hiyo wanaifanya kwa kutembea kwa miguu porini.
“Kazi ya kupiga sumu kwa mikono ni ngumu na tunatembea kilometa 80 kwa siku kuwafuatilia nzige maporini ili kuwaua wote pia mawasiliano huku porini ni magumu hatuna radio calls” alisema Muro
Naye Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Zephania Chaula aliwapongeza wataalam wa kilimo kwa kazi nzuri ya kuwadhibiti nzige tangu walipoingia kwenye wilaya yake na kuwa sasa hakuna kundi linaloonekana angani baada ya kupuliziwa sumu.
Chaula alishukuru pia vyombo vya habari kwa kazi nzuri ya kuelimisha na kuufahamisha umma hali iliyosaidia hofu miongoni mwa wananchi kupungua juu ya madhara ya nzige kwa kuwa hatua za kuwadhibiti zimeonekana.
“Pongezi kwa vyombo vya habari kwa kutoa taarifa sahihi zinazosaidia kudhibiti makundi ya nzige sasa wananchi wanafahamu tupo kwenye vita na wanatuunga mkono kwa kutupa taarifa pale nzige wanapoonekana kwenye maeneo yao” alisema Chaula.
Mwenyekiti wa kijiji cha Landanai wilaya ya Simanjiro Joshua Ombya Marite alisema wameshuhudia nzige wamekufa kwenye maeneo mengi kijiji hapo baada ya ndege kunyunyiza sumu na kuwa wanaomba zoezi hilo serikali iendelee ili waishe wote kabisa na malisho ya mifugo yasipotee.
Banaska Munga ambaye ni Mtendaji wa Kijiji cha Losokonoi wilaya hiyo ya Simanjiro alisema wameshirikiana kwa karibu na wataalam wa kudhibiti nzige kwa kuwaonyesha njia maporini kujua makundi ya nzige walipotua na pia kufuatia kujua endapo wamekufa.
Munga aliongeza kusema “wataalam wa wizara ya kilimo wanatembea maporini kuanzia saa 12 asubuhi hadi usiku kufuatilia nzige tukiwa pamoja kwa kuwa tunataka wote wafe ili majani ya mifugo yetu yasiliwe na wadudu hawa” alisema Mtendaji huyo wa Kijiji cha Losokonoi.