………………………………………………………………………………………………..
Na Mwamvua Mwinyi,Pwani
Chemba ya wafanyabiashara mkoani Pwani (TCCIA ) ,imefanya uchaguzi baada ya uongozi uliopita kutenguliwa kutokana na kushindwa kuwa imara ambapo Saidi Yusuph Mfinanga amechaguliwa kuwa Mwenyekiti mpya wa chemba hiyo.
Uongozi huo mpya uliochaguliwa unatarajia kwenda kuiokoa chemba hiyo ambayo iliyumba kwa miaka mitatu kwa kutofanya mikutano na wanachama,mahesabu tete na uongozi kutoelewana.
Makamu mwenyekiti wa TCCIA kilimo makao makuu -Joseph Kaungwa ,alisema menejimenti ya awali ilivunjwa kuanzia Januari mwaka huu,licha ya kufanya uchaguzi halali kikatiba.
Alieleza kwamba ,kwasasa baada ya kuwa chini ya usimamizi wa TCCIA makao makuu ,wamefanya uchaguzi mpya kwa chemba ya Pwani ili iweze kuimarika.
“Uongozi uliopita haukuwa na ushirikiano ,mahesabu hayakufanyiwa ukaguzi na hawakueleweka ,tulitafakari na kuona haiwezi kuendelea kwa kuyumba namna ile acha ufanyike uchaguzi na kupata viongozi ambao wataiinua TCCIA Pwani ” alifafanua Kaungwa.
Alieleza ,viongozi hawa wapya wanapaswa kuweka mikakati madhubuti ya kuondoa doa na mapungufu yaliyojitokeza .
Kaungwa aliwaelekeza viongozi hao ,chini ya mwenyekiti mpya Saidi Mfinanga kuhakikisha wanaandaa taarifa ya chemba na mipango yao ndani ya miezi sita .
Akishukuru wapiga kura ,Saidi Mfinanga alisema atatumia elimu na uzoefu wake kuwawezesha wafanyabiashara mkoani Pwani kufanya biashara zao kwa kuweka mahesabu na kutoa mafunzo mbalimbali juu ya masuala ya mahesabu na biashara.
Nae makamu mwenyekiti Biashara TCCIA Pwani ,Fadhili Gonzi ,alisema wafanyabiashara wengi wanafeli na biashara zao kufa kutokana na elimu ya fedha na namna ya kujiwekea akiba
“Mali bila daftari hupotea bila habari, wafanyabiashara tujali faida na hesabu za biashara zetu ,nitashirikiana na wadau kutoa elimu hii ili tunufaike na kuinua uchumi wetu” alibainisha Fadhili.
Katika uchaguzi huo waligombea nafasi ya mwenyekiti walikuwa wawili akiwemo Joseph Njile aliyepata kura 20 na Saidi Mfinanga aliyeshinda kwa kupata kura 67.
Nafasi nyingine ni Kilimo,wajumbe wa mkutano mkuu wa Taifa TCCIA Pwani na biashara.