…………………………………………………………………………………………
Na. Angela Msimbira DAR-ES-SALAAM
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli amewaagiza Viongozi wa Sekretarieti za Mkoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kutumia muda wao kutatua kero za wananchi na sio kuacha hadi wananchi wasubirie viongozi ngazi ya kitaifa wakija ndio waltatuliwe kero zao.
Akiweka jiwe la msingi katika Soko la Kisasa la Kisutu Halmashauri ya Jiji la Dar-es-salaam Mhe. Magufuli amesema kumekuwa na wimbi kubwa la wananchi kusubiri viongozi wa ngazi ya Kitaifa ili kuweza kutatuliwa kero zao, jambo ambalo halihitajiki katika kipindi hiki cha awamu ya tano.
Mhe. Magufuli amesema kuwa Wakuu, wa Mikoa, wakuu wa Wilaya, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wilaya, wakurugenzi, watendaji wa kata, watendaji wa vijiji na mitaa wanawajibu wa kuhakikisha wanatatua kero za wananchi kwa haraka na wakati kwa kuwapatia majibu sahihi na kumaliza kero zao.
“Inasikitisha kuona wananchi wakipata shida kutoa mabango, na kuleta kero zao kwenye mikutano kama hii, haileti tija kwa nchi, wananchi wanahitaji kupata majibu ya kero zao kwa wakati, viongozi ngazi ya Mamlaka za Serikali za Mitaa hakikisheni mnatatua kero hizo zisinifikie” amesisitiza Mhe. Magufuli
Akiweka Jiwe la Msingi katika Soko la Kisutu Mhe. Magufuli amemtaka Mkandarasi kuhakikisha wanakamilisha ujezi wa soko kwa wakati uliopangwa ili liweze kutoa huduma kwa wananchi.
Amesema kuwa ujenzi wa masoko ni kiungo muhimu katika kukuza uchumi wa nchi kwa kuwa kupitia masoko wakulima wanapata sehemu ya kuuzia mazao yao nakupata bei ya uhakika.
Aidha, Mhe. Magufuli amefafanua kuwa Soko hilo litasaidia kuinua uchumi wa eneo husika, kuhusisha wafanyakazi wengi na kurahisisha shughuli zao za kufanyabishara katika Jiji la Dar-es-salaam.
Wakati Huohuo Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa mhe. Selemani Jafo amesema kuwa ujenzi wa Soko la Kisasa la kisutu umegharimu kiasi cha shilingi Bilioni 13.4 ambapo kwa sasa litaweza kuwa na wafanyabishara 1500.