*****************************
Wataalam wa elimu, afya na ustawi wa jamii katika Manispaa ya Ilemela wamejengewa uwezo wa kubaini, kuchukua hatua na kupambana na vitendo vya ukatili, ulinzi na usalama kwa watoto wenye umri wa kuanzia miaka tisa hadi kumi na nne kupitia vipindi vya michezo na dini mashuleni.
Mafunzo hayo yamelenga kuwaanda vijana kuwa wanaume bora ‘Coaching Boys Into Men’ CBIM kupitia mradi wa BORESHA ili waweze kutambua na kuheshimu haki zao na za watu wengine pamoja kupinga vitendo vya kikatili na unyanyasaji kwa ajili ya kujenga jamii iliyo sawa na yenye kuwajibika
Akizungumza wakati wa mafunzo ya kuwajengea uwezo walimu hao, afisa elimu michezo wa Manispaa ya Ilemela Mwalimu Kizito Bahati Sosho alisema kuwa wanafunzi watakapopata ufahamu juu ya vitendo vya kinyanyasaji na ukatili itawasaidia wao kujilinda na kuvipinga vitendo hivyo.
‘.. Tunategemea wanafunzi wetu watakapopata ufahamu juu ya vitendo vya kinyanyasaji na ukatili itasaidia wao wenyewe kuchukua hatua za kupinga vitendo hivi vya kinyanyasaji kwao wenyewe na kwa watu wengine ..’ Alisema
Aidha afisa ustawi wa jamii wa Manispaa ya Ilemela Bi Stella Mbura akaongeza kuwa Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kudhibiti vitendo vya ukatili kwa watoto na unyanyasaji ikiwemo kuanzisha timu za ulinzi na usalama wa watoto (MTAKUWWA) kwa ngazi ya mitaa, kata na wilaya.
Pamoja na jitihada hizo alisema kuwa zipo ofisi za ustawi wa jamii ambazo hutumika kwa ajili ya kutoa taarifa matukio mbalimbali ya kikatili na unyanyasaji huku wakishirikiana na vituo vya polisi kupitia dawati la jinsia na watoto na mashirika mbalimbali ambayo husaidia kutoa msaada wa kisheria pamoja na elimu ya kuzuia matendo ya aina hiyo.
Kwa upande wake mratibu mwandamizi kutoka shirika la TIP (Tanzania Interfaith Partnership) Ndugu Shukuru Mohammed alisema kuwa mradi wa BORESHA unatekelezwa katika wilaya tatu za Ilemela, Kwimba na Buchosa mkoani Mwanza huku ukitekeleza afua ya UKIMWI ambapo una vipaumbele viwili cha kwanza ni kuhimiza wakinababa na wavulana kupima ili kujua hali zao za kiafya na ya pili ni kumlinda mtoto kwa maana ya watu wenye umri chini ya miaka 18 ambapo afua hizi kubwa mbili zimebeba afua ndogo ndogo ikiwemo afua ya mafunzo ya kumfanya mvulana kuwa mwanaume bora ‘Coaching Boys Into Men’ CBIM.
Aliongeza kuwa afua hii imekusudia kumjengea mtoto uwezo wa kujitambua nafasi yake kuwa mtu mzima na kuthamini usawa wa kijinsia ambapo afua hii itaendeshwa kupitia vipindi vya dini na michezo vya kila wiki mashuleni kwa wanafunzi wa kiume kuwekwa katika makundi ya idadi ya watoto arobaini wakifundishwa namna ya kujiepusha na kuripoti vitendo vya ukatili, unyanyasaji wa kijinsia na baadae kushiriki michezo kwa pamoja vyote vikibeba dhima ya kupambana na ukatili.
Nae moja ya washiriki wa mafunzo hayo Mwalimu Frida Mollel kutoka shule ya msingi Kirumba iliyopo kata ya Kirumba akaishukuru serikali na shirika la kijamii la TIP kwa kuja na mpango huu wa mafunzo ya kuwaanda vijana kuwa wanaume bora kwani utawasaidia kujitambua hivyo kupunguza vitendo vya ukatili na unyanyasaji katika jamii
Mafunzo haya yameendeshwa na Serikali kwa kushirikiana na wadau kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali ya TIP, AGPAHI na WORLD VISION kwa mafunzo kwa baadhi ya maafisa wa idara ya elimu msingi, ustawi wa jamii, afya na walimu wa shule 35 zilizopo ndani ya wilaya hiyo, shule 30 zikiwa za Serikali na shule 5 zinazomilikiwa na watu binafsi.