Sehemu mojawapo ya daraja la Kankwale iliyoanza kumeguka kutokana na mmomonyoko kabla ya daraja hilo kumalizika huku mafundi wakiendelea kuona namna ya kudhibiti hali hiyo isiendelee.
mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akionesha mahala ambapo kumeendelea kumeguka (hakupo pichani) katika daraja hilo linaloendelea kujengwa la Kankwale lenye thamani ya Shilingi milioni 238.
Mstahiki Meya wa manispaa ya Sumbawanga Justin Malisawa (kushoto) akitoa maelezo juu ya athari za mmomonyoko katika daraja la Kankwale lililopo kata ya Sumbawanga Asilia kwa wajumbe wa bodi ya barabara mkoani Rukwa.
Daraja la Momoka lililopo kata ya Momoka, Manispaa ya Sumbawanga ambalo magari yamezuiwa kupita kutokana na kuharibika kwake na kusababisha adha kwa wananchi wenye usafiri huo.
………………………………………………………………………………….
Wakati mvua zikiendelea kunyesha mkoani Rukwa na kuharibu baadhi ya miundombinu ya barabara na madaraja mkoani humo, shughuli za kibinaadamu zinazofanyika kando ya mito na barabara zimeendelea kuongeza ugumu wa kutunza miundombinu hiyo na hatimae kuisababishia serikali kupoteza fedha nyingi kwaajili ya kuirekebisha badala ya kujenga mipya.
Hayo yameonekana baada ya wajumbe wa bodi ya barabara mkoani Rukwa kufanya ziara fupi katika daraja la kankwale lililopo kata ya Sumbawanga Asilia Pamoja na daraja la momoka lililopo katika kata Momoka yanayounganisha viunga vya mji wa Sumbawanga kabla ya kufanyika kwa kikao cha bodi hiyo.
Wakizungumza katika nyakati tofauti wajumbe wa bodi hiyo ambao pia ni wabunge katika majimbo ya mkoa wa Rukwa wamesema kuwa kushughulika na chanzo cha uharibifu wa miundombinu hiyo itakomesha uharibifu huo.
Akitoa maoni yake Mbunge wa jimbo la Kalambo Mh. Josephat Kandege amesema kuwa kwa muda mrefu binadamu wamekuwa wakiingilia mikondo ya maji na hivyo kusababisha maji hayo kuhama na matokeo yake kuharibu miundombinu iliyosimikwa katika meneo husika.
“Kwa vyovyote vile itakuwa katika vyanzo vya maji, ukiwauliza wazee wa zamani watakwambia mkondo halisi wa maji ni hapa sasa, kwaajili ya shughuli za binadamu tunataka tulazimishe sehemu ambazo ni za maji kupita tunafanya shughuli zetu, angalia mahindi yamelimwa mpaka hapo,” Alisema.
Kwa upande wake Mratibu wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Rukwa Mhandisi Seth Mwakyembe aliiomba serikali kuiongezea TARURA fedha lakini pia aliwaomba wabunge wa mkoa kusukuma maombi yao ya bajeti itakayowawezesha kumalizia miradi iliyopo.
“Kubwa zaidi tunaiomba serikali Pamoja na waheshimiwa wabunge kusisitiza kuiongezea TARURA fedha za kukamilisha miradi iliyopo hasa ya mkoa wa Rukwa, Mkoa wetu wa Rukwa kuna shida kubwa sana za mmomonyoko katika kingo za mito na madaraja kwahiyo tunaamini kabisa kwamba bajeti tuliyoandaa ni nzuri ambayo ikipitishwa na waheshimiwa wabunge tutafanya kazi kwa ufanisi,” Alisema.
Aidha, Diwani wa kata ya Momoka Mchungaji Gerald Chakupewa aliiomba serikali kuhakikisha daraja linalounganisha kata hiyo ya Momoka na mji wa Sumbawanga linatengenezwa kwa wakati.
“Maana asilimia 80 ya wakazi wa Momoka wanalitegemea daraja hili kwenda kufanya shughuli zao za kimaendeleo, ukiangalia hata huko chini, daraja limeanza kuachia na tulikuwa tumeshaweka zuio hapa ili wananchi wasipite lisije likatokea jambo lolote hapa lakini watu wanaendelea kupita na hatuna namna yoyote lakini tunaomba msaada,” Alisema.
Katika Kuhakikisha jambo hilo linashughulikiwa Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amemuagiza Mkurugenzi wa manispaa ya Sumbawanga kutumia sheria ndogo za halmashauri Pamoja na sheria za mazingira kuhakikisha wanaokika sheria hizo wanashughulikiwa bila ya kufyeka mazao yao.
“Niseme tu wananchi wetu wazingatie sheria, kanuni na taratibu zinazopiga marufuku kulima kwenye vyanzo vya maji, ili kuokoa rasilimali, fedha nyingi zimetumika hapa, kuna mamilioni, hili daraja limetumia milioni 200 na kitu, ni wananxhi hawa hawa daraja likiharibika ndio wanaopiga kelele kuwa barabara hazitengenezwi, madaraja hayatengenezwi lakini wanalima kwenye vyanzo vya maji, badala ya kuzui wao wanabomoa,” Alisisitiza.
Daraja la Kankwale limegharimu shilingi milioni 238 na limeanza kumomonyoka kabla ya kumalizika huku mkandarasi akiwa ameshalipwa Shilingi milioni 167.3 na kutarajiwa kumaliza tarehe 28.2.2021, hapo hapo daraja la Momoka likiwa limeharibika kiasio cha magari kushindwa kupita huku TARURA wakiwa wamelitengea daraja hilo bajeti ya Shilingi milioni 270 katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 na kuhamisha ujenzi wa daraja katika eneo jingine.