Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akifurahia jambo wakati akiagana na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Albert Chalamila wakati wa ziara yake ya siku moja katika mkoa wa Mbeya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasishaji ukusanyaji kodi ya pango la ardhi tarehe 23 Februari 2021.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi, Wakuu wa wilaya na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Mbeya wakati wa kikao cha kazi kuhusiana na masuala ya sekta ya ardhi na kuhamasishaji ukusanyaji kodi ya pango la ardhi tarehe 23 Februari 2021. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Paul Ntinika.
Sehemu ya Wakurugenzi wa Halmashauri za mkoa wa Mbeya na Watendaji wa Sekta ya ardhi wakimsikiliza Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara yake ya siku moja katika mkoa wa Mbeya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi na kuhamasishaji ukusanyaji kodi ya pango la ardhi tarehe 23 Februari 2021.
Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mbeya Siyabumi Mwaipopo akizungumza wakati wa kikao cha kazi baina ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula na Watendaji wa sekta ya ardhi na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Mbeya kuhusiana na masuala ya sekta ya ardhi na kuhamasishaji ukusanyaji kodi ya pango la ardhi tarehe 23 Februari 2021.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi hati za ardhi mkazi wa Ubaruku Mbarari mkoa wa Mbeya Bi. Asha Manasi alipogawa hati wakati wa kikao cha kazi na Watendaji wa sekta ya ardhi na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Mbeya kuhusiana na masuala ya sekta ya ardhi na kuhamasishaji ukusanyaji kodi ya pango la ardhi tarehe 23 Februari 2021.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwa katika picha ya pamoja na wananchi aliowakabidhi hati za ardhi mkoani Mbeya wakati za ziara ya kikazi kuhamasishaji ukusanyaji kodi ya pango la ardhi tarehe 23 Februari 2021. Wa pili kulia waliokaa ni Mkuu wa Wilaya ya Mbeya Mjini Paul Ntinika na wa pili kushoto waliokaa ni Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mbeya Siyabumi Mwaipopo. (PICHA ZOTE NA MUNIR SHEMWETA)
************************************
Na Munir Shemweta, WANMM MBEYA
Ofisi ya Ardhi mkoa wa Mbeya kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya ya Mbarari imeanza kutekeleza mradi wa usajili ardhi vijijini katika vijiji 20 vya halmashauri ya Mbarari kama mradi wa mfano unaotarajiwa kutekelezwa katika halmashauri zote za mkoa wa Mbeya.
Mradi huo unatekelezwa kwa kutumia mfumo wa kisasa wa upimaji na uchukuaji picha za anga ambapo wanufaika wake wanachangia gharama za kupanga, kupima na kumilikishwa vipande vyao kwa kuzingatia dhana ya fit for purpose.
Hayo yamebainishwa jijini Mbeya tarehe 23 Februari 2021 na Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mbeya Siyabumi Mwaipopo alipowasilisha taarifa ya sekta ya ardhi katika mkoa wake katika kikao baina ya Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula na Watendaji wa sekta ya ardhi pamoja na wakurugenzi wa halmashauri za mkoa wa Mbeya.
‘’Uchangiaji gharama za kupanga, kupima na kumilikisha ardhi katika mradi huu una mambo mawili ya msingi ambayo ni kuondoa dhana ya utegemezi katika utoaji huduma za ardhi nchini pamoja na kufanya umilikishaji ardhi kuwa endelevu’’ alisema Siyabumi.
Kwa mujibu wa Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Mbeya, katika kutekeleza mradi huo wananchi wanaomiliki ekari 1 mpaka 10 watachangia shilingi 30,000 na wale wenye mashamba ya ukubwa wa ekari 11 mpaka 50 watachangia shilingi 60,000 huku wenye ekari kuanzia 51 na kuendelea wakichangia 120,000.
Alisema, kupitia mradi huo jumla ya vijiji 10 kati ya 20 vya mradi vitapimwa mipaka yake na ramani kusajiliwa, vijiji 13 vitaandaliwa mipango ya matumizi ya ardhi, vijiji 4 ambavyo mipango ya matumizi bora ya ardhi inakaribia kuisha muda wake mipango yake itarejewa upya , vyeti vya ardhi vya vijiji 10 vitaandaliwa katika eneo la mradi na kila kipande cha ardhi kitapimwa na kupatiwa hati miliki ya kimila.
Aidha, aliongeza kuwa, katika utekelezaji mradi huo taasisi zote za kisheria zinazohusika na migogoro ya ardhi zitajengewa uwezo kwa kupatiwa mafunzo bora ya ya uendeshaji mabaraza ya ardhi ya vijiji na kata zote zilizo eneo la mradi. Pia Mabaraza ya Ardhi ya vijiji 8 yataanzishwa katika eneo la mradi sambamba na Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Mbarari kuanza kufanya kazi mapema.
Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi katika halmashauri za wilaya katika mkoa wa Mbeya kuanza kutoa elimu ya kupanga maeneo katika vijiji ili kuepuka ujenzi holela.
‘’Tuanze kutoa elimu kwa watendaji walioko vijijini, wajue ABC za kupanga maeneo yao kabla hayajaanza kutangazwa maeneo ya upangaji na tukifanya hivyo miji yetu itakaa vizuri na tutaondokana na zoezi la urasimishaji ambalo linamalizika 2023’’ alisema Dkt Mabula.
Katika hatua nyingine, Naibu Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula aliagiza kufuatiliwa kwa wamiliki wote wa viwanja wenye tozo ya adhabu ya maendelezo yaliyokiuka sheria ya mipango miji katika mkoa wa Mbeya ili waweze kulipa kiasi wanachodaiwa kama walivyopelekewa ilani za madai.
Kwa mujibu wa Taarifa ya sekta ya ardhi, mkoa wa Mbeya una idadi ya viwanja 154 ambavyo wamiliki wake wamefanya maendelezo kwa kukiuka masharti ya uendelezaji na viwanja hivyo vinadaiwa kiasi cha shilingi 1,074, 830,060.00 huku 65,100,000.00 pekee ndizo zilizolipwa.