Home Mchanganyiko HOSPITALI YA TUNDURU YAANZA KUPIMA KIFUA KIKUU WAHUDUMU WA BAR

HOSPITALI YA TUNDURU YAANZA KUPIMA KIFUA KIKUU WAHUDUMU WA BAR

0
Mratibu wa kifua kikuu na ukoma wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Dkt Mkasange Kihongole akizungumza na baadhi ya wahudumu wa Bar maarufu ya Laprasido wilayani humo wakati  akifungua kampeni ya uelimishaji na uhamasishaji  wa ugonjwa wa kifua kikuu wilayani humo.

Picha na Muhidin Amri

*******************************

 Na Mwandishi Maalum
RUVUMA

KUTOKANA na wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kuongoza kwa  maambukizi  makubwa ya ugonjwa wa kifua mkoani Ruvuma,Hospitali ya wilaya yaTunduru kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma imeanza  kampeni ya kudhibiti  ugonjwa huo kwa kutoa elimu ya uelimishaji na uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa huo kwa wahudumu wote wa Bar.

Mratibu wa kifua kikuu na Ukoma wa wilaya hiyo Dkt Mkasange Kihongole amesema,  wamelazimika kuwafikia  wahudumu wa Bar kwa kuwa ni kati ya makundi hatarishi  kutokana na kuishi na kufanya kazi kwenye mikusanyiko na kukutana na watu wengi  mara kwa mara.

Alisema, katika kampeni hiyo inayojulikana kwa jina la Kilinge kwa kilinge,nyumba kwa nyumba na shule kwa shule wanatarajia kuzifikia Bar,Grocery na vilabu vyote vinavyouza pombe kwa ajili ya kutoa elimu  na kufanya uchunguzi wa ugonjwa huo kwa watoa huduma na watu wengine watakaokutwa katika maeneo hayo.

Dkt Mkasange ametoa kauli hiyo jana wakati akizindua rasmi elimu ya uhamasishaji, uelimishaji na uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu kwa wahudumu wa Bar wilayani Tunduru uliofanyika  katika Bar  maarufu ya Laprasido wilayani humo.

Alisema, mbali na wahudumu wa Bar  makundi mengine yalioko katika hatari ya kupata ugonjwa wa kifua kikuu ni wasafiri,wanywa pombe kupindukia,wazee,wanafunzi wanaoishi bweni,watu wanaofanya shughuli zao kwenye misongamano na wafugaji.

Alitaja watu wengine wanaoweza kupata kifua kikuu kwa urahisi ni wale  wote wenye magonjwa yanayosababisha kushuka kwa kinga mwilini kama ukimwi,kisukari,kansa,utapiamlo kwa watoto na watu wazima,wasio na makazi maalum ambao wanalazimika kulala zaidi ya watu watano katika sehemu moja,umaskini au hali duni ya kipato na wanaotumia dawa bila kupata ushauri wa mtaalam.

Alisema, TB ni ugonjwa unaoenea kwa njia ya hewa kutoka kwa mtu mwenye vimelea vya ugonjwa huo ambaye hajaanza  tiba kwenda kwa mtu mwingine kwa kupiga chafya, kutema mate ovyo au makohozi.

Alisema, vimelea vya TB  kwa kawaida ushambulia mapafu na vina uwezo wa kushambulia viungo vyote vya mwili isipokuwa nywele,meno na kucha.

Alitaja dalili za mtu mwenye kifua kikuu ni kukohoa kwa wiki mbili  na zaidi,homa za mara kwa mara kwa wiki mbili  na kuendelea,kutokwa  jasho jingi usiku, kukohoa makohozi yenye damu,kupungua uzito,kukosa hamu ya kula, kwa mtoto kukosa raha na kulia lia,kupungua uzito au kudumaa na kupumua kwa shida.

Amewataka wahudumu hao kuchukua tahadhari na kuwa na utaratibu wa kuchunguza afya zao mara kwa  mara na kwa wale watakaobainika kuwa na ugonjwa huo wataanzishiwa matibabu ambayo yanatolewa bure katika zahanati,vituo vya Afya na Hospitali zote za Serikali hapa nchini.

Aidha, amewashauri wahudumu hao na jamii kuhakikisha watoto wanachomwa  chanjo ya BCG mara baada ya kuzaliwa,kuziba pua na mdomo kwa kitambaa au mikono unapokohoa au kupiga chafya,kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuimarisha kinga za mwili.

Mkasange alisema,njia nyingine za kujikinga na kifua kikuu ni kula vyakula vyenye virutubisho vyote muhimu kwa afya bora,kutumia dawa kinga kwa wale walio kwenye hatari ya kuambukizwa,kuepuka mikusanyiko au mirundikano ya watu na kuishi kwenye nyumba yenye mfumo mzuri wa hewa.

Baadhi ya wahudumu  wa Bar wameiomba Serikali kuendelea kutoa elimu na huduma ya uchunguzi kwa wahudumu mara kwa mara kwani itasaidia kuepuka kupata ugonjwa huo kutoka kwa watu wengine wanaofika katika shughuli zao.

Emeliana Komba muhudumu wa Bar ya Laparsido alisema,elimu waliyoipata imewasaidia kufahamu ugonjwa wa kifua kikuu na jinsi ya kuchukua  tahadhari na kuepuka kupata maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu.

Meneja wa  Bar ya Terminal Ali Pinde alisema, changamoto kubwa  kwa wahudumu ya Bar ni kukutana na watu tofauti mara kwa mara pamoja na suala zima la kuishi watu zaidi ya watano katika chumba kimoja.
MWISHO.