Picha na Muhidin Amri
Na Mwandishi Maalum
RUVUMA
KUTOKANA na wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma kuongoza kwa maambukizi makubwa ya ugonjwa wa kifua mkoani Ruvuma,Hospitali ya wilaya yaTunduru kupitia kitengo cha kifua kikuu na ukoma imeanza kampeni ya kudhibiti ugonjwa huo kwa kutoa elimu ya uelimishaji na uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa huo kwa wahudumu wote wa Bar.
Mratibu wa kifua kikuu na Ukoma wa wilaya hiyo Dkt Mkasange Kihongole amesema, wamelazimika kuwafikia wahudumu wa Bar kwa kuwa ni kati ya makundi hatarishi kutokana na kuishi na kufanya kazi kwenye mikusanyiko na kukutana na watu wengi mara kwa mara.
Alisema, katika kampeni hiyo inayojulikana kwa jina la Kilinge kwa kilinge,nyumba kwa nyumba na shule kwa shule wanatarajia kuzifikia Bar,Grocery na vilabu vyote vinavyouza pombe kwa ajili ya kutoa elimu na kufanya uchunguzi wa ugonjwa huo kwa watoa huduma na watu wengine watakaokutwa katika maeneo hayo.
Dkt Mkasange ametoa kauli hiyo jana wakati akizindua rasmi elimu ya uhamasishaji, uelimishaji na uchunguzi wa vimelea vya ugonjwa wa kifua kikuu kwa wahudumu wa Bar wilayani Tunduru uliofanyika katika Bar maarufu ya Laprasido wilayani humo.
Alisema, mbali na wahudumu wa Bar makundi mengine yalioko katika hatari ya kupata ugonjwa wa kifua kikuu ni wasafiri,wanywa pombe kupindukia,wazee,wanafunzi wanaoishi bweni,watu wanaofanya shughuli zao kwenye misongamano na wafugaji.
Alitaja watu wengine wanaoweza kupata kifua kikuu kwa urahisi ni wale wote wenye magonjwa yanayosababisha kushuka kwa kinga mwilini kama ukimwi,kisukari,kansa,utapiamlo kwa watoto na watu wazima,wasio na makazi maalum ambao wanalazimika kulala zaidi ya watu watano katika sehemu moja,umaskini au hali duni ya kipato na wanaotumia dawa bila kupata ushauri wa mtaalam.
Alisema, TB ni ugonjwa unaoenea kwa njia ya hewa kutoka kwa mtu mwenye vimelea vya ugonjwa huo ambaye hajaanza tiba kwenda kwa mtu mwingine kwa kupiga chafya, kutema mate ovyo au makohozi.
Alisema, vimelea vya TB kwa kawaida ushambulia mapafu na vina uwezo wa kushambulia viungo vyote vya mwili isipokuwa nywele,meno na kucha.
Alitaja dalili za mtu mwenye kifua kikuu ni kukohoa kwa wiki mbili na zaidi,homa za mara kwa mara kwa wiki mbili na kuendelea,kutokwa jasho jingi usiku, kukohoa makohozi yenye damu,kupungua uzito,kukosa hamu ya kula, kwa mtoto kukosa raha na kulia lia,kupungua uzito au kudumaa na kupumua kwa shida.
Amewataka wahudumu hao kuchukua tahadhari na kuwa na utaratibu wa kuchunguza afya zao mara kwa mara na kwa wale watakaobainika kuwa na ugonjwa huo wataanzishiwa matibabu ambayo yanatolewa bure katika zahanati,vituo vya Afya na Hospitali zote za Serikali hapa nchini.
Aidha, amewashauri wahudumu hao na jamii kuhakikisha watoto wanachomwa chanjo ya BCG mara baada ya kuzaliwa,kuziba pua na mdomo kwa kitambaa au mikono unapokohoa au kupiga chafya,kufanya mazoezi mara kwa mara ili kuimarisha kinga za mwili.
Mkasange alisema,njia nyingine za kujikinga na kifua kikuu ni kula vyakula vyenye virutubisho vyote muhimu kwa afya bora,kutumia dawa kinga kwa wale walio kwenye hatari ya kuambukizwa,kuepuka mikusanyiko au mirundikano ya watu na kuishi kwenye nyumba yenye mfumo mzuri wa hewa.
Baadhi ya wahudumu wa Bar wameiomba Serikali kuendelea kutoa elimu na huduma ya uchunguzi kwa wahudumu mara kwa mara kwani itasaidia kuepuka kupata ugonjwa huo kutoka kwa watu wengine wanaofika katika shughuli zao.
Emeliana Komba muhudumu wa Bar ya Laparsido alisema,elimu waliyoipata imewasaidia kufahamu ugonjwa wa kifua kikuu na jinsi ya kuchukua tahadhari na kuepuka kupata maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu.
Meneja wa Bar ya Terminal Ali Pinde alisema, changamoto kubwa kwa wahudumu ya Bar ni kukutana na watu tofauti mara kwa mara pamoja na suala zima la kuishi watu zaidi ya watano katika chumba kimoja.
MWISHO.