Home Mchanganyiko WAKULIMA KISIWANI PEMBA KUPATA FURSA YA KUJIFUNZA MBINU ZA KILIMO BORA

WAKULIMA KISIWANI PEMBA KUPATA FURSA YA KUJIFUNZA MBINU ZA KILIMO BORA

0

Mabwana na Mabibi Shamba kutoka Wilaya nne za Pemba wakiwa katika mafunzo ya vitendo ya kuanzisha mashamba darasa -picha na Masanja Mabula-

****************************************

Na Masanja Mabula, PEMBA.

WATAALAMU wa Kilimo Kisiwani Pemba  wametakiwa  kuanzisha mashamba darasa kwa wakulima ili kutoa fursa ya wakulima kujifunza mbinu mpya za kilimo chenye tija na kuleta mabadiliko chanya ya kilimo katika maeneo yao.

Katibu Tawala Wilaya Ndogo Kojani Makame Khamis Makame aliwasisitiza wataalamu hao wa kilimo kutumia taaluma yao kufanya utafiti wa udongo hali itakayo wawezesha wakulima  kutambua aina ya udongo  sambamba na aina ya mbegu lengo ni kuongeza uzalishaji.

 Hayo aliyasema wakati akifunga mafunzo ya siku tano ya  kilimo cha Viungo , Mboga Mboga na Matunda kwa mabwana na mabibi shamba kisiwani Pemba,

Alisema kutokana na changamoto hiyo wakulima wengi wanalima bila ya kuwa na taaluma sahihi ya akutumia mbegu zinazoendana na udongo na hivyo kusababisha kukosa tija kwa kilimo.

“Mafunzo haya yakawe chachu ya kuleta mabadiliko chanya ya kilimo , kwa kusimamia zaidi unzishwaji wa mashama darasa katika maeneo yenu”alisisitiza.

Meneja wa mradi wa viungo, mboga mboga na matunda Sharif Maalim Hamad amesema mradi huo unatarajia kuwanufaisha wakulima 21,000 Unguja na Pemba huku wengi wao na wanawake.

“Mradi huu unatarajia kuwanufaisha wanawake 21,000. Ikiwa 10,500 ni kutoka Pemba na waliobaki watatoka Unguja”alisema.

Aidha aliwataka mabwana na mabibi shamba kuhakikisha wanawake wanashiriki kwa wingi katika mashamba darasa ili kutoa fursa ya kupata taaluma za kilimo.

Washiriki wa mafunzo hayo wameahidi kutamia mafunzo hayo kuimarisha mashamba darasa ambayo ni sehemu sahihi ya wakulima kupata taaluma ya kilimo.

Mradi huo pia ni suluhisho ya changamoto ya soko la bidhaa za zitokanazo la mboga mboga,viungo pamoja na matunda.