Home Mchanganyiko TUMIENI VIAPO VYENU KUJENGA IMANI YA WANANCHI KWA MAHAKAMA – JAJI KIONGOZI

TUMIENI VIAPO VYENU KUJENGA IMANI YA WANANCHI KWA MAHAKAMA – JAJI KIONGOZI

0

Baadhi ya Mahakimu Wakazi wakifuatilia mafunzo elekezi yanayoendelea Chuoni Lushoto.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akifungua mafunzo elekezi kwa Mahakimu Wakazi II wapatao 71 (hawapo pichani) yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto.

Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmillah Sarwatt akitolea ufafanuzi wa jambo wakati mafunzo elekezi kwa Mahakimu Wakazi II wapatao 71 (hawapo pichani) yanayofanyika Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto.

Mkurugenzi wa Rasilimaliwatu na Utawala Mahakama ya Tanzania Bw. Edward Nkembo akitolea ufafanuzi taratibu za ajira wakati wa mafunzo hayo.

Kaimu Naibu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto Bi. Mwanabaraka Mnyukwa akitolea ufafauzi kuhusu maandalizi ya mafunzo elekezi kwa Mahakimu Wakazi II wapatao 71 (hawapo pichani).

***********************************

Na Innocent Kansha, Mahakama – Lushoto.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amewataka Mahakimu Wakazi wapya 71 kuamua mashauri kwa kuzingatia viapo vyao vinavyowataka kutenda haki pasipo kuangalia rangi, dini, chama, umri wala jinsia ya mtu.

Akifungua mafunzo elekezi kwa Mahakimu hao yanayofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto mkoani Tanga mapema leo Februari 22, 2021, Mhe. Jaji Kiongozi alisema maamuzi ya mashauri yatakayofanywa na Mahakimu hao lazima yazingatie sheria, ushahidi uliopo na miongozo ya kimahakama na si vinginevyo.

 “Msiamue mashauri hayo kwa chuki, huba, tetesi, hisia, kwa misukumo na mihemko mbalimbali, nendeni mkawe mwarobaini wa kutoa suluhisho kwenye maeneo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wananchi katika Mahakama za Mwanzo”, alisisitiza Jaji Kiongozi.

Mhe. Jaji Dkt. Jaji Feleshi aliyataja mashauri hayo ambayo ni mashauri ya mirathi, mgawanyo wa mali za ndoa, matunzo na hifadhi ya watoto pia kukazia na kutimiza hukumu huku akiongeza kuwa wajibu wao kuwa makini na kuchukua tahadhari kwakuwa maamuzi mabaya juu ya maeneo haya huumiza makundi maalumu yanayohusisha wototo, wajane, wagane na wazee, halikadhalika huondoa imani ya wananchi kwa Mahakama.

Aidha, Mhe. Jaji Kiongozi aliwakumbusha Maafisa hao wa Mahakama kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuharibu taswira ya Mahakama kama matumizi ya lugha chafu, kujigeuza Mungu mtu, mavazi yasiyozingatia maadili ya kazi, ufuska, ubabaishaji, ulevi, kuchelewa kuanza Mahakama, kuingilia au kuhoji maswali wakati kesi ikiendelea kwa kiwango cha kupitiliza, kuchelewesha maamuzi na kutotoa nakala za hukumu mambo haya ni kinyume kabisa na maadili ya utumishi wa Mahakama.

Kwa upande mwingine, Mhe.Jaji Kiongozi aliwahimiza Mahakimu hao wapya kujinoa zaidi kwenye matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) na mifumo ya kielektroniki inayotumika mahakamani ili waweze kuendana na kasi ya mabadiliko ya kidunia. Raha ya uafisa wa Mahakama wa sasa ni pamoja na kuwa na ujuzi na uelewa wa kutosha katika matumizi ya TEHAMA. Pia kutumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kuongeza tija na manufaa ya Mahakama na Taifa kwa ujumla.

Aidha, Dkt. Feleshi aliwakumbusha Maafisa kuzingatia matumizi sahihi ya Lugha katika utendaji kazi wa kila siku. Msiache kujisomea stadi za lugha na kukuza misamiati kwani mashauri mengi kushughulikiwa na Mahakama za Mwanzo inawapa wigo mpana wa kukuza lugha ya Kiswahili cha kisheria.

Halikadhalika, Jaji Kiongozi aliwasisistiza Maafisa hao kutojitenga na wananchi na mamlaka zinazoongoza kuanzia ngazi ya mashina, Vijiji, Kata na Tarafa kwa kisingizio cha kulinda Uhuru wa Mahakama. Viongozi wa maeneo haya husika ni walinzi wa amani na pia ni wadau muhimu sana wa Mahakama.

Kwa upande mwingine Jaji Kiongozi aliwahimiza Mahakimu Wakazi hao kumaliza mashauri ndani ya muda usiozidi miezi mitatu na kuzingatia lengo la kumaliza mashauri 260 kwa mwaka. Kwa kufanya hivyo watafikia lengo la kutenda haki kwa wote na kwa wakati.

Kwa upande wake, Makamu Naibu Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama – Lushoto, Bi. Mwanabaraka Mnyukwa alisema Chuo kinayapa mafunzo haya umuhimu mkubwa kikitambua kuwa dhamana waliyopewa Mahakimu wapya sio ndogo na inahitaji weledi na uadilifu mkubwa na mafunzo ni sehemu muhimu ya kuwafanya watimize jukumu hilo kwa ukamilifu.

“Tukumbuke kuwa kuhukumu ni kazi ya Mungu na kwa duniani Jaji na Hakimu ndio wamepewa jukumu hilo na hivyo ni wajibu wetu sote kufanya vile Mungu atapendezwa nasi”, alisistiza Makamu Naibu Mkuu wa Chuo.

Aidha, Bi Mnyukwa katika nukuu yake alisema “Vitabu vya dini vinasema kuna Mahakimu/Jaji wa aina tatu. Mmoja ataingia Peponi na wawili wataenda Motoni. Aliyehukumu watu kwa kuijua haki na kuifuata huyo ataishia Peponi. Na ataye hukumu watu kutokana na ujinga (kwa kutojua haki) huyo ataishia Motoni na mtu anayehukumu watu kwa dhulma (anayejua haki lakini akapindisha) ataishia Motoni.”

Jumla ya Mahakimu wakazi wapya 71 waliaapishwa Februari 18, 2021 na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es Salaam.