………………………………………………………………………
Na.Alex Sonna
Wawakilishi pekee ukanda wa Afrika Mashariki na Kati Timu ya Simba imezidi kujichimbia kileleni mwa Msimamo wa Kundi A wa Michuano ya klabu bingwa Afrika hatua ya makundi baada ya kuwachapa bao 1-0 Mabingwa watetezi Al Ahly kutoka Misri Mechi iliyopigwa uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam.
Simba ilipata bao la ushindi kupitia kwa winga hatari kutoka Msumbiji Luis Miquissone dakika ya 29 kwa shuti kali lililomshinda mlinda mlango wa Al Ahly na kutinga nyavuni.
Matokeo mengine ya kundi hilo Timu ya Al-Merreikh ya Sudan limezidi kuzama baada ya kukubali kichapo cha pili mfululizo kwa kufungwa nyumbani Mabao 4-1 na wageni As Vita ambao walipoteza mechi ya kwanza nyumbani kwa kufungwa na Simba bao 1-0.
Kwa Matokeo hayo Simba wamefikisha Pointi 6 na kuongoza kundi A huku nafasi ya pili ikishikwa na As Vita kwa Pointi 3 sawa Al Ahly wenye pointi 3 nafasi ya tatu huku Al-Merreikh wakiburuza mkia wakiwa hawana Pointi timu zote zikiwa zimecheza mechi mbili.
Chama la Simon Msuva timu ya Wydad Casablanca wamepata ushindi wa ugenini kwa kuwafunga wenyeji Petro Atletico ya Angola bao 1-0 lililofungwa na Ayoub El Kaabi dakika ya 71 mchezo wa kundi C.
Kundi hilo majira ya saa moja kamili Kaizer Chiefs watakuwa uwanja wa nyumbani kucheza na timu ya Herieth Makambo nyota wa zamani wa Yanga kutoka Guine timu ya Horoya AC.