Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania Balozi Stephen P. Mbundi akichangia jambo kwenye Mkutano wa 40 Wakawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki unaofanyika jijini Arusha, Tanzania.
Sehemu ya washikiri kutoka Tanzania wakifuatilia Mkutano wa 40 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki unaondelea jijini Arusha.
Mkutano ukiendelea
Meza kuu kutokea kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Mipango, Miundombinu, Fedha na Utawala Mhandisi Steven Mlote, Naibu Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala uzalishaji na sekta ya kijamii Christophe Bazivamo na Mshauri wa Masuala ya Jumuiya Dkt. Antony L. Kafumbe wakifuatilia mkutano.
Sehemu nyingine ya washiriki wa mkutano wakifuatilia majadala uliokuwa ukiendelea
…………………………………………………………………………………..
Mkutano wa 40 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki umeendelea kufanyika kwa siku ya pili leo jijini Arusha. Mkutano huo utakaofanyika kwa kipindi cha siku nne (4) (tarehe 22 hadi 25 Februari 2021) utafanyika katika ngazi tatu, ambazo ni; ngazi ya Wataalam (tarehe 22-23 Februari), ngazi ya Makatibu Wakuu (tarehe 24 Februari) na ngazi ya Mawaziri (tarehe 25 Februari). Mkutano huu unafanyika kwa njia ya ana kwa ana na video.
Miongoni mwa masuala yaliyopo kwenye agenda ni pamoja uwasilishwaji wa ripoti mbalimbali ikiwemo ripoti za utekelezaji wa maamuzi mbalimbali ya Baraza la Mawaziri, Ofisi ya Katibu Mkuu wa Jumuiya, Mipango na Miundombinu na Sekta ya Uzalishaji na Huduma za Jamii.
Sambamba na hayo masuala mengine yatakayo jadiliwa ni kuhusu; Siasa, Forodha na Biashara; Masuala ya Fedha na Utawala; na Ripoti ya Taasisi zingine zilizopo chini ya Jumuiya zikiwemo Bunge la Afrika Mashariki na Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki.
Baraza pia linatarajiwa kujadili na kupitisha agenda na ratiba iliyopendekezwa ya Mkutano wa 21 wa Wakuu wa Nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki uliopangwa kufanyika Jumamosi, 27 Februari, 2021.
Baraza la Mawaziri la Afrika Mashariki ni Chombo kinachounda Sera za Jumuiya. Baraza hili linaundwa na Mawaziri wanaosimamia Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na/au Ushirikiano wa Kikanda kutoka Nchi Wanachama.
Mjukumu mengine ya Baraza hili ni ufuatiliaji, uangalizi na usimamizi wa utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Jumuiya na kuhakikisha utendaji mzuri wenye tija wa Taasisi zingine za Jumuiya.
Ujumbe wa Tanzania kwenye Mkutano huu katika ngazi ya wataalamu unaongoza na Mkurugenzi wa Siasa, Ulinzi na Usalama kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Stephen Mbundi.