Meneja Usimamizi wa watoa huduma ndogo za kifedha na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni Bw.Victor Tarimu akiwasilisha mada katika Semina kwa Waandishi wa Habari za Fedha, Uchumi na biashara inayofanyika Mkoani Mtwara.
*************************************
Benki Kuu ya Tanzania BOT imesema hakuna tozo yoyote ya vikundi vidogo vya kifedha vya kijamii (VICOBA) vinavyoendesha shughuli zake, na kwamba hakuna kikundi chochote cha kifedha kinachomilikiwa na Benki hiyo.
Benki hiyo pia imesema vikundi vya kifedha vya Kijamii ni mali ya Wanachama na kwamba hakuna kikundi kinacholazimika kuwa chini ya makundi mengine kama SACCOS na Taasisi za kifedha.
Hayo yamebainishwa na Meneja Usimamizi wa watoa huduma ndogo za kifedha na maduka ya kubadilisha fedha za kigeni Bw.Victor Tarimu wakati akitoa mada katika Semina kwa Waandishi wa Habari za Fedha, Uchumi na biashara inayofanyika Mkoani Mtwara.
“Hakuna fedha inayotozwa na Benki Kuu ya Tanzania-BOT kwa ajili ya uendeshaji wa kikundi vya kifedha, na hakuna sheria yoyote inayotaka vikundi hivyo vitoe tozo kwenye Taasisi nyingine yoyote, vikundi ni mali ya wanachama na wanaotoza vikundi hivyo kwa ajili ya uendeshaji wanakosea” alisema Bw.Tarimu.
Aliyasema hayo baada ya Waandishi wa Habari kumwambia kuwa kuna baadhi ya Halmashauri za Wilaya na Manispaa wanatoza vikundi hivyo Shilingi elfu 30 kama gharama za uendeshaji wa vikundi.
“BOT tuliwaambia Mamlaka za Halmashauri za Wilaya kuwa, mnaposajili kundi dogo la kifedha, hakuna kutoza pesa yoyote, kama kuna kundi lipo linatozwa fedha sh elf 30 za usajili watuambia, na sisi tutachukua hatua kwa sababu sio utaratibu tuliowapa”alisema
Alisema kutokana na kuona kuna umuhimu mkubwa wa makundi hayo ya Kijamii kujikwambua kiuchumi kupitia mzunguko wa fedha zao wenyewe, BOT iliamua vikundi hivyo visajiliwe bure na kusisitza kuwa Halmashauri za Wilaya wanalifahamu jambo hilo.
Hata hivyo alisema kuwa Sekta ndogo ya fedha ni miongoni mwa sekta muhimu kwa wananchi wa kipato cha chini inayosaidia kuongeza kipato na kupunguza umasikini.
Pamoja na hayo amesema vitu vya msingi kanuni za watoa huduma ndogo za fedha kanuni 2019 zinajumuisha masharti ya uanzishaji wa kikundi (kanuni za 4-7) ambapo mkutano wa awali, kamati ya mpito na majukumu yake pamoja na kikao cha uanzishaji na majukumu yake.