Home Mchanganyiko DIWANI LUKA AISHAURI HALMASHAURI SIMANJIRO KUWAPONGEZA WALIMU

DIWANI LUKA AISHAURI HALMASHAURI SIMANJIRO KUWAPONGEZA WALIMU

0
****************************************
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
DIWANI wa Kata ya Endiamtu wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Lucas Chimbason Zacharia, ameishauri Halmashauri ya Wilaya hiyo kuweka utaratibu wa kuwapongeza walimu na wanafunzi waliofanya vizuri katika matokeo ya mitihani ili kuwatia moyo katika utendaji kazi na kuleta matokeo mazuri zaidi katika matokeo yajayo.
Luka akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani amesema  kufanya hivyo kutawasaidia kuongeza juhudi na kuleta matokeo chanya zaidi.
Amesema zipo kata ambazo shule zake zimefanya vizuri katika matokeo ya kidato na nne na cha pili, na hata matokeo ya matokeo ya darasa la saba, ikiwemo kata yake ya Endiamtu.
“Sasa ni vyema  halmashauri ikaona umuhimu wa kuzipongeza ili walimu waweze kutiwa moyo wa kuongeza jitihada zaidi za kufaulisha huku nao  wanafunzi walioachwa mashuleni wakiendelea na masomo wapate hamasa ya kuongeza juhudi katika masomo,” amesema Luka.
Amesema huu ndiyo wakati wa halmashauri ya Simanjiro kuweka utaratibu wa kuwapongeza walimu waliofaulisha vizuri wanafunzi pia kuwapongeza wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao ili kuleta hamasa katika utendaji wao wa kazi, na hatimaye waweze kuongeza juhudi zaidi.
Ametolea mfano katika  shule ya sekondari Mirerani Benjamini Mkapa kwa matokeo ya kidato cha nne imefaulisha daraja la kwanza wanafunzi tisa, daraja la pili wanafunzi 27, daraja la tatu wanafunzi 21 na daraja la nne 63, matokeo ambayo hayajawahi kutokea tangu shule hiyo ilipoanza kufaulisha mwaka 2002.
Amesema hata matokeo ya kidato cha pili yaliyotoka, waliopata daraja la kwanza ni wanafunzi 38, daraja la pili wanafunzi 29, daraja la tatu wanafunzi 47, daraja la nne wanafunzi 58 na daraja 0 ni wawili.
“Sasa hapa ndio narudi palepale halmashauri yetu ya Simanjiro tukiweka utaratibu wa kuwapongeza walimu na wanafunzi na shule zilizofanya vizuri,  hata matokeo yajayo hayatakua kama haya,” amesema Luka.
Amesema endapo wakipongezwa lazima matokeo yatakua mazuri zaidi ya haya, hivyo anawapongeza walimu na wanafunzi waliofanya vizuri katika matokeo yaliyopita.
Hata hivyo amewataka walimu na wanafunzi waongeze bidii zaidi kwani hata wale ambao hawakufaulu, watafaulisha wanafunzi na wao kwa sasa hawawezi kukaa kimya lazima watatafuta mbinu mbadala iliyowafanya wanafunzi wafeli, hivyo walimu wahakikishe wanakuwa na mbinu tofauti tofauti za ushindi.
“Walimu wetu binafsi kama diwani wa kata ya Endiamtu natambua kazi nzuri zinazofanywa na walimu wote katika kata yangu, ninachowaomba tuhakikishe mnasimama kikamilifu na wanafunzi wote kwa pamoja ili mwakani tuweze kufaulisha zaidi ya waliofaulu sasa,” amesema Luka.
Ametoa hongera kwa walimu wa Wilaya ya Simanjiro na kuwapa moyo waendelee kuongeza bidii zaidi ya matokeo hayo ili hata kwa mwaka huu wa 2021 kuwe na matokeo mazuri kwa wanafunzi wote.